26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU: NAPE SI JAMBAZI

EVANS MAGEGE Na ASHA BANI

-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu, atumie picha kumsaka mtu ambaye alitumia silaha ya moto aina ya bastola kumtisha aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, asizungumze na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa ujumbe uliosambaa jana asubuhi kwenye mitandao ya kijamii ambao Mwigulu alilithibitishia gazeti hili kuwa ni wake, alisema mtu huyo alifanya kitendo cha uhalifu kwa kofia ya uaskari.

Alifafanua kwamba, iwapo mtu huyo atabainika kuwa ni askari, basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake.

“Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania. Nape Moses Nnauye si jambazi,  ni Mtanzania, ni Mbunge, Mjumbe wa NEC ya CCM, hana rekodi ya uhalifu. Kitendo cha mtu kumtolea bastola si cha kiaskari, si cha Kitanzania na si cha ki-Mungu, kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera nawaza mbali kwamba ingekuwa kwenye kichochoro angefanya nini,” anatanabahisha Mwigulu.

Wakati Waziri huyo wa Mambo ya Ndani akitoa msimamo huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Susan Kaganda,  amekanusha kuzuia mkutano wa Nape na waandishi wa habari uliokuwa ufanyike katika Hoteli ya Protea, iliyoko Oysterbay, Dar es Salaam.

Kaganda, ambaye jana alikuwa akizungumza katika kipindi cha Maisha Mseto, kinachorushwa na Radio Times Fm, alisema hakutoa maelekezo ya kuzuia mkutano wa Nape na kwamba kufika kwake katika eneo lile ilikuwa ni kuangalia hali ya usalama inaimarika zaidi.

Alisema Protea ni hoteli ya mtu binafsi na si mali ya Serikali na kwamba ni biashara huru, hivyo hawezi kuzuia, licha ya kwamba alikutana na kundi la waandishi na kuzungumza na baadhi yao.

Aliongeza kuwa, yeye kazi yake ni kusimamia usalama wa raia na mali zao na kwamba  mkutano ungemhusu kama ungekuwa wa hadhara na si vinginevyo.

Alipoulizwa kuhusiana na kipande cha picha jongefu (video) inayomwonesha mtu anayedhaniwa kuwa askari akimtolea silaha Nape, alisema hawezi kuongelea suala hilo kwa sasa hadi uchunguzi utakapokamilika, kwa maana video hiyo haikuonyesha sura ya mhusika.

Alisema Jeshi la Polisi linawafundisha askari  kutumia nguvu kwa namna wanavyokutana na mazingira.

“Nilifika kumuuliza Nape kama yupo salama na kisha nikaondoka…lakini kama kuna silaha imetumika kama ambavyo nimeona kwenye vyombo vya habari, tunalifanyia uchunguzi, sikuwapo eneo la tukio na picha ile inaonyesha kisogo, kuweni watulivu tunachunguza,’’ alieleza Kaganda.

Juzi Nape aliandaa mkutano katika Hoteli ya Protea akiwa na lengo la kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na sakata zima linaloendelea, likiwamo la kuondolewa katika nafasi yake ya uwaziri, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Dk. Harrison Mwakyembe.

Kabla ya kuingia katika mkutano huo, saa nane Meneja wa Hoteli aliyejulikana kwa jina moja la Suleiman aliwaambia waandishi wa habari kuwa, alipokea simu kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kaganda akimtaka asiruhusu kufanyika kwa mkutano huo.

Baadaye baada ya kutokea purukushani za kushikiwa bastola, alifanikiwa kuzungumza na waandishi wa habari, hata hivyo, wakati anaondoka gari alilokuwa amepanda RPC Kaganda lilifika na kulizuia gari lake kwa mbele.

Baada ya mazungumzo kati yao, baadaye Nape aliwaaga waandishi wa habari, akisema anaelekea nyumbani kwake na kisha gari lake na lile ya polisi kuondoka kila mmoja akielekea njia yake.

Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa, wengi wakilaani na kutaka mtu aliyemnyooshea bastola Nape kuchukuliwa hatua mara moja.

Kagasheki

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi wakati wa Utawala wa Awamu ya Nne, Balozi Khamis Kagasheki, aliandika ujumbe katika mtandao wa Twitter uliosomeka:  Tanzania haiko chini ya utawala wa kijeshi.

Balozi Kagasheki, ambaye alilithibitishia gazeti hili kuwa ndiye aliyeuandika ujumbe huo, alifafanua kwamba, askari kumtolea bastola raia ambaye hana silaha yoyote haikubaliki na si kitendo cha kufurahia.

Askofu Kilaini

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini, alisema tukio la askari kumtisha Nape kwa bastola ni geni tangu uhuru wa nchi hii, hivyo limesababisha jamii kushangaa kwa kiasi kikubwa.

Katika maelezo yake, alisema tatizo hilo si la Taifa au Jeshi la Polisi nchini, bali ni tatizo la mtu binafsi.

Kwa mantiki hiyo, aliziomba mamlaka za ulinzi kumchukulia hatua mtu huyo aliyemtisha Nape kwa bastola hadharani.

“Sijui alikuwaje huyu jamaa aliyetoa bastola, hata kama unamshurutisha mtu basi walau msukume na si kutumia bastola kwa sababu bastola ni kifo. Ikitokea bahati mbaya unatisha ikatoka risasi…unakumbuka ile kesi ya Iringa kuhusu marehemu Daudi Mwangosi,” alisema Askofu Kilaini.

Sheikh Alhadi

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salumu, alisema wanajiandaa kutoa tamko kama viongozi wa dini.

“Tuna kamati ya amani, hivyo tunakutana kwa ajili ya kulizungumza hili na tutatoa tamko hivi karibuni, kwa hiyo kwa sasa sitaweza kusema zaidi,” alisema Sheikh Alhadi.

Askofu Mwasota

Katibu mstaafu wa Makanisa ya Kipentekoste  nchini, Askofu David Mwasota, alisema kitendo cha askari kumtisha Nape kwa bastola si cha kiungwana.

Askofu Mwasota alisema kitendo hicho kinaibua tafsiri nyingi juu ya kilichokuwa nyuma ya utashi wa askari huyo kama aliamriwa au shetani alitaka kumtuma.

“Siyo haki kwa binadamu kutishiwa silaha ya moto, viongozi wa dini tuungane kwa pamoja kuliombea Taifa na kumtaka Mungu ashushe busara ili mambo kama haya yasijirudie,” alisema Askofu Mwasota.

Ole Ngurumwa

Naye Mratibu wa Mtandao wa Wapigania Haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa, alisema kitendo  hicho ni kosa baya kwa upande wa Serikali.

Alisema hatari ya kimakosa kuhusu tukio la aina hiyo inataka kufanana na makosa yaliyotendeka siku za nyuma na kusababisha mauaji yaliyomkuta marehemu Mwangosi.

“Kwa mfano, kama risasi ingefyatuka tayari Nape angekuwa amepoteza maisha bila ulazima, sisi tunalaani vitendo vya namna hiyo na tunaomba aliyefanya hivyo achukuliwe hatua  na iwe ni mwisho kwa askari wa namna hiyo kutoa silaha pale ambapo wanaona hapafai kutoa kwa sababu pale hapakuwa na fujo na watu hawakuwa na silaha.

“Tutatoa tamko siku chache zijazo, kwa sasa tunafanya utafiti zaidi ili kuandika ushahidi wa kina kwa haya mambo yanayoendelea kujitokeza nchini,” alisema Ole Ngurumwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles