Na PETER FABIAN
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amewataka watanzania kuunga mkono kwa dhati juhudi za Rais Dk John Magufuli katika mapambano dhidi ya vita ya uchumi, rasilimali za taifa, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma.
Kauli hiyo alitoa Mwanza wakati akiwa mgeni rasmi katika hafla ya harambee ya kuchangia fedha za ujenzi wa kituo cha televisheni, radio na studio ya kurekodia cha Gombo kusaidia kutangaza Injili cha Kanisa la EAGT Mwanza.
Kituo hicho kiliasisiwa na Hayati Askofu Dk. Moses Kulola.
Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) aliwashauri viongozi wa dini, watumishi wa Mungu na Watanzania wote waendelee kumuombea rais wakati huu akiwa kwenye mapambano hayo ya uchumi, kutetea na kulinda rasilimali za taifa ziweze kulinufaisha na kuwa na maendeleo.
Alisema serikali ya Rais Magufuli imeanza kuwachukulia hatua mbalimbali kwa watuhumiwa wa ufisadi na wahujumu uchumi na inaendelea kuchukua hatua.
Waziri alisema wapo baadhi ya watu na wanasiasa wamekuwa wakitumia maneno yenye viashiria vya uchochezi, kubeza na kumdhalilisha rais na serikali ya awamu ya tano kwa juhudi izinazochukuliwa kusimamia, kutetea na kulinda rasilimali za taifa kuwa watakutana na mkono wa sheria.
“Si kila kauli ni za siasa na maisha ya watanzania hayana siasa hivyo ni vema kabla ya kuzitoa kauli hizo wazitafakari kama zina tija kwa wananchi.
“Hakuna siasa katika kulinda rasilimali zote za taifa bali ni jukumu la watanzania kuweka kando tofauti za itikadi na kushirikiana na serikali iliyopo madarakani kuzilinda,”alisisitiza.
Waziri alisema uchangiaji wa ujenzi huo utaendelea hadi kazi ya kukamilisha itakapofikia uzinduzi rasmi wa kituo hicho.
Alisema yeye na marafiki zake walichangia Sh milioni 20 za kuanzia huku akiendesha mnada wa vitu ambavyo marehemu Askofu Kulola aliagiza kupigwa mnada kuchangia ujenzi huo.
Awali mtoto wa marehemu Askofu Kulola, Willy Kulola ambaye ni mkurugenzi wa kituo hicho alisema ziara ya Waziri Nchemba ni kutekeleza maagizo ya marehemu baba yake Kulola.
Mjane wa marehemu Askofu Kulola, Elizabeth Kulola alisema aliagizwa kumkabidhi vitu waziri huyo ili kusaidia kuvinadi na kuendesha harambee kusaidia kufanikisha kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.