27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU ASEMA POLISI HAWATEKI WATU

Na GABRIEL MUSHI, DODOMA


WABUNGE wameitaka Serikali kuwachukulia hatua watu ‘wasiojulikana’ pamoja na kukomesha vitendo vya utekaji na uteswaji kwa kuwa vinalichafua Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Jeshi la Polisi haliteki watu kama inavyodaiwa na baadhi ya Watanzania wakiwamo wabunge.

Hayo yalijiri bungeni jana jijini Dodoma wakati wabunge wakijadili Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo pamoja na mambo mengine wabunge walisema vitendo hivyo vimejenga hofu ndani ya jamii.

Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM), alisema matukio yanayotendwa na watu wasiojulikana hayaathiri upinzani pekee kama inavyodaiwa bali pia imewaathiri na wanachama wa CCM.

Alisema ana uhakika na taarifa hizo kwa kuwa anayo orodha ya wana CCM waliodhuriwa na watu wasiojulikana.

Kauli ya Maige ilimwuibua Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), ambaye alimpa taarifa na kubainisha kuwa idadi ya watu waliotendwa na watu wasiojulikana ni wengi.

Hata hivyo, Kabla Maige hajaendelea kuchangia, Waziri mwenye dhamana Dk. Nchemba alisimama na kusema Jeshi la Polisi halijateka watu. “Mheshimiwa Maige anaongelea watu wasojulikana” alisema.

Hali hiyo iliendelea kuzua mvutano ambapo Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisimama na kusema suala la uhalifu, halilinganishwi kwa vyama vya siasa kwa kuwa Jeshi la Polisi linalinda usalama wa raia wote.

Akiendelea kuchangia mjadala huo, Maige alisema anazungumzia watu wanaofanya matukio na  hawakamatwi  na hazungumziai suala la uhalifu.

Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Yusuph (Chadema), alisimama na kumpa taarifa Maige kuwa suala la kusema matukio yaliyofanyika upande wa upinzani na CCM hayafanani, inadhihirisha kwamba CCM na Serikali imebariki mfumo na matukio hayo.

Aidha, akihitimisha mjadala huo, Maige alisema. “Mimi nashangaa upande ule (wa upinzani) wanakurupuka, mimi naongelea ombi langu kwa Serikali ili kuweza kuwakamata watu wasojulikana,”  alisema.

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), alimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, kutumia nguvu alizonazo kimamlaka kuwashughulikia watu wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuwachafua viongozi.

Alisema matusi mitandaoni yamejaa na haijulikani rais ni nani, kiongozi ni nani ilihali akaunti zinazotukana zinajulikana.

“IGP (Sirro) tumekuweka nyota mabegani tumia nguvu zako” alisema.

Aidha, alisema asilimia 85 ya huduma inayotolewa na Jeshi la Polisi inahusisha rushwa.

Wakati Mbunge wa Viti Maalum, Fakharia Shomar Khamis (CCM), alisema licha ya majukumu makubwa waliyonayo polisi lakini vitendea kazi vyao sio rafiki na sehemu wanazofanyia kazi si rafiki.

Mbunge wa wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema), katika mchango wake alimtaka Dk. Nchemba kusimamia weledi wa Polisi ili kuondoa dhana ya kutokuaminika kwa jamii.

Alisema kuna mambo yanafanyika nchini ikiwamo mtu aliyedaiwa kumtishia kwa bastola Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), hadi sasa hajachukuliwa hatua licha ya ahadi ya waziri ya kushughulikiwa jambo hilo.

“Hivi huyu mtu haonekani. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo amekamatwa ofisini kwake, tena amekamatwa na DCO, polisi wako kimya… Matukio haya yanafanya jeshi kuonekana halina weledi, vilevile RPC wa Iringa anasema Abdul Nondo alikwenda mwenyewe hakutekwa. Kanda Maalum ya Dar es Salaam inasema alikamatwa sasa tuwaelewe vipi?

“Hawa polisi wamesoma mbona hamfanyi kazi kwa weledi? Nchi yetu ilikuwa ya amani lakin mnafanya mambo yasiyotakiwa. Juzi juzi RPC wa Arusha alipata ajali watu wanasema bora afe, tusifike huko,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalum, Alfredina Kahigi (CUF), alisema kufuatia matukio ya watu kutekwa na kuteswa watu wanahofu inayowafanya wasiwe na amani.

“Watu wanatekwa, wanauawa kwa sababu ya mambo ajabu. Nasikitika sana kwa haya yanayotokea, Serikali yangu ichukue hatua haraka,” alisema.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles