RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MBUNGE wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) amesimulia jinsi punda walivyotaka kupoteza uhai wake, huku mara kwa mara akisema. “Mungu ni mwema”.
Mbunge huyo alipata ajali hiyo jana katika eneo la Migori barabara ya Dodoma –Iringa wakati akielekea mkoani Singida.
Akizungumza kwa taabu akiwa amelazwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini hapa, Mwigulu alisema anamshukuru Mungu kwa kutoka mzima kwani dereva wake aligonga punda waliokuwa wakivuka barabara.
“Nilikuwa natokea Iringa naenda Singida kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa, sikuwa naangalia mbele nadhani nilikuwa naongea na simu kama sikosei, ghafla wakakatiza punda kama sikosei walikuwa watatu.
“Nilishtuka tu dereva alivyotoa ishara kwamba kuna kitu cha hatari, ilikuwa ni kitendo cha kufumbua macho hapo hapo na gari ikawa imepinduka.
“Waligongwa wale watatu lakini mmoja alikuwa anamalizia barabara na mwingine alikuwa anaanza barabara, mwingine alikuwa katikati kwahiyo hakukuwa na sehemu ya kukwepea.
“Nilisikia kelele moja kubwa sana ya kugonga na baada ya hapo sikuona tena mbele kwa sababu ghafla niliona mbele yangu pamekuwa padogo sana na kulikuwa na moshi.
“Mwanzo sikuona kama nimeumia sana nikamuuliza mwenzangu unaendeleaje? nikamwambia tunaweza kutoka akaniambia ngoja kwanza kwani moshi ulikuwa mkubwa sana, nikawa naona kama vile kuna hitilafu kubwa ya moto kwani kulikuwa na moshi sana na nilikuwa nimebananishwa sana,”alisema Mwigulu.
Mwigulu alisema alipotoka ndani ya gari aliona kifua kinambana huku akisikia maumivu makali katika mguu wa kulia.
“Nilipotoka kifua kilikuwa kinauma, kiuno na mguu. Nashukuru nimepokelewa hapa na nimepewa huduma haya maumivu ya kubana yaliyokuwa yakinisumbua naona sio sana yamebaki maumivu ya mwili tu,”alisema.
Mwigulu ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema anamshukuru Mungu kwa kutoka salama kwani alikuwa akiona kifo kipo mbele yake.
Akizumgumzia dereva alisema hali yake ni nzuri na aliwaagiza wasaidizi wake wampigie kujua hali yake.
Mwigulu aliwataka Watanzania kuendelea kumwombea ili aweze kupona. “Naomba waniombee Mungu ni mwema ametunusuru, Mungu ni mwema ametunusuru,”alisema Mwigulu kwa taabu.
DEREVA
Kwa upande wake dereva wa gari hiyo, Johnson Malesi akizungumza kwa njia ya simu na MTANZANIA alisema ajali hiyo ni kama ya maajabu kwani imetokea katika eneo la wazi.
Alisema ilitokea majira ya saa 2:45 asubuhi katika eneo la migori mkoani Iringa, ambapo alidai alikuwa akikwepa punda waliotokea ghafla barabarani.
“Ilkuwa majira ya saa 2:45 asubuhi tulikuwa tunatokea Iringa kupitia barabara ya Mtera na tulikuwa tumefika Migori na tulikuwa tumeachana na kijiji kulikuwa hakuna makazi ya watu.
“Ghafla likatokea kundi la punda ambao walikuwa wanavuka barabara na walikuwa wakikimbia, nilipojaribu kuwakwepa ilishindikana nikamgonga mmoja ambaye ndiye aliyesababisha ajali,” alisema.
Alisema kwenye gari walikuwa yeye na Mwigulu hivyo mara baada ya ajali kutokea, waliangaliana na kusaidiana kutoka nje ya gari.
“Tulikuwa wawili tu kwenye gari na baada ya ajali nikafungua mlango akashuka, akanifungulia mlango akaniuliza huna mchubuko wowote, nikamwambia sina lakini baadae akaanza kulalamika maumivu,”alisema dereva huyo.
Alisema baada ya hapo alikuwa akilalamika maumivu katika mguu, hivyo akaomba msaada wa gari iliyokuwa ikipita kwa ajili ya kumleta Dodoma kwa matibabu.
“Tulivyoshuka ikapita gari ya Serikali nikaisimamisha na nikawaambia tunaomba msaada ndio wakatusaidia,” alisema.
Dereva huyo alisema anamshukuru Mungu kwani hakuumia mahali popote kutokana na kufunga mkanda.
“Namshukuru Mungu naendelea vizuri wala sijapata maumivu yoyote, tulikuwa tumefunga mkanda hivyo ilivyopinduka haikuwa shida na gari haikutoka nje ya barabara,”alisema
DAKTARI
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dk.Alfonce Chandika, alisema walimpokea Mwigulu majira ya saa tatu asubuhi.
Alisema mbunge huyo anaendelea vizuri na wamempima ndani ya mwili na kugundua hakuna madhara makubwa ambayo ameyapata.
“Kwa sasa yupo vizuri tulichokifanya tulimpeleka kwenye vipimo hasa kile cha CT Scan, tulikuwa tunataka kujua ni maeneo gani ameumia. Tumempatia dawa za maumivu hali yake inaendelea vizuri,”alisema Dk.Chandika.
NAIBU WAZIRI
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Musa Sima, alikuwa kiongozi wa kwanza wa Serikali kufika kumjulia hali Mwigulu.
Sima ambaye ni Mbunge wa Singida Mjini (CCM), alisema alikuwa safarini kuelekea Morogoro na mara baada ya kupata taarifa hiyo, alifika kumjua hali Mwigulu.