26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

Mwenyekiti wenye ualbino alia kuitwa majina ya ajabu

Na AHMED MAKONGO

– BUSEGA

IMEELEZWA licha ya matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino kupungua, bado wapo baadhi ya watu katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, wamekuwa wakiwaita majina ya ajabu ya kuwanyanyapaa, hali inayowasononesha na kuwanyima raha ndani ya jamii inayowazunguka.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) wilayani Busega, Mihayo Lilanda, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ngasamo, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.

Mkutano huo, pamoja na mambo mengine ulikuwa ni kwa ajili ya kutoa elimu ya ustawi wa jamii na kupinga vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino, kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na jamii kujua haki za wazee.

Uliandaliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Nabroho yenye makao yake makuu wilayani hapa.

Lilanda aliyataja baadhi ya majina ambayo  wamekuwa wakiitwa kuwa ni pamoja na Mbilimwilu (yaani mbuzi mweupe), Zeruzeru (yaani fisi mweupe), dili, mtu wa mkosi, mtu wa laana na mtu wa Msimbazi (yaani noti ya shilingi elfu kumi).

“Baadhi ya watu wamekuwa wakituita sisi watu wenye ualbino majina ya ajabu sana. Wengine wanatuita eti sisi Mbilimwilu, yaani mbuzi mweupe, majina mengine wanatuita eti Zeruzeru yaani fisi mweupe, mara tunaitwa dili, mtu aliye na mkosi, mtu mwenye laana na kwamba sisi ni Msimbazi, yaani ile noti ya shilingi elfu kumi,” alisema kwa masikitiko Lilanda.

Alisema majina hayo yanawakosesha raha na kujiona kwamba siyo binadamu wa kawaida wakati wao pia ni watu kama wengine.

Aliiomba jamii iachane na tabia ya kuwanyanyapaa kwani wao pia ni binadamu na wanao uwezo wa kufanya kazi kama walivyo watu wengine.

Ofisa Tathmini wa Asasi ya Nabroho, Zabron John, alisema watu wenye ualbino ni binadamu kama wengine na hivyo haipo haja ya kuwanyanyapaa, kwani wanastahili haki zote za msingi, ikiwemo kutowatenga katika masuala mbalimbali ya kijamii.

John alisema wapo baadhi ya watu wenye ualbino wana elimu nzuri na wengine wanazo shughuli zao muhimu za kuwaongezea kipato, hivyo jamii isiwaone wao siyo watu wa kawaida kwani hayo ni maumbile waliyozaliwa nayo na wala hayasababishi mkosi wowote kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa na imani za kishirikina kwamba viungo vya mtu mwenye ualbino vinasababisha utajiri au kupata uongozi na kwamba siyo kweli kwani hiyo ni imani potofu na kuwataka watu waachane nazo.

 “Ualbino siyo mkosi wala mtu mwenye ualbino siyo kwamba kiungo chake au nywele zake zitakupatia utajiri au kupanda cheo au kupata uongozi, hizo ni imani potofu na za kijinga sana.

“Sasa tumekuja hapa kutoa elimu kwa wananchi ili wote kwa pamoja tujue kuwa watu wenye ualbino ni kama sisi… mbona kuna watu wengine wanazo kasoro kadhaa, wengine wana mapengo mbona hao hamuwasemi?” alihoji.

Aliongeza kuwa; “baadhi ya watu wanaendekeza imani za kishirikina kwa kudhani kwamba viungo vya albino vitampatia utajiri na kwamba ilifikia hatua watu hao wakaanza kuwasaka hata watu wenye vipara, hizo ni imani za kijinga.”

Kutokana na hilo aliwataka wana jamii kuachana na ramli chonganishi kwani ni chanzo cha kuwepo mauaji ya watu wenye ualbino kwa imani za kishirikina na pia kuwepo kwa mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Alifafanua kuwa baadhi ya watu wenye imani ya kishirikina wamekuwa na imani za ajabu ikiwa ni pamoja na kuamini mtu akifanya mapenzi na mtu mwenye ualbino hawezi kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi jambo ambalo si kweli.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani hapa, Grace Mmasi, aliwataka wananchi kuachana na imani potofu kwani hali hiyo inarudisha maendeleo yao nyuma, ambapo pia aliwataka wananchi kujiunga kwenye vikundi vikiwemo vya watu wenye ualbino, ili waweze kukopesheka na kuwasaidia kujiinua kiuchumi na kujiletea maendeleo zaidi.

Akizungumzia sera ya wazee ya mwaka 2003, Mmasi alisema bado haijatungiwa sheria na kusema iwapo hilo litafanyika masuala ya wazee yatakwenda vizuri na kuzipata haki zao zote stahiki.

Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kufika kwenye mkutano huo, akiwemo Anna Simon, waliishukuru Nabroho kwa kuwapa elimu hiyo, na Halmashauri ya Busega kutoa huduma ya matibabu bure kwa wazee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles