28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mwenyekiti wa Ukawa afariki dunia

makaidiJONAS MUSHI, DAR NA FLORENCE SANAWA, MTWARA

MWENYEKITI mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk. Emmanuel Makaidi, amefariki dunia.

Dk. Makaidi ambaye alikuwa akigombea ubunge katika Jimbo la Masasi mkoani Mtwara kupitia Chama cha NLD alichokuwa mwenyekiti wake, alifariki dunia jana saa 7:15 mchana katika Hospitali ya Nyangao, mkoani Lindi alikokuwa akitibiwa.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Meneja wa kampeni za Makaidi, Faraji Mangochi, alisema kabla hajapelekwa hospitalini jana saa 5:15 asubuhi, Dk. Makaidi aliishiwa nguvu ghafla akiwa nyumbani kwake Masasi na kuanguka kutokana na shinikizo la damu lililokuwa likimsumbua.

Akizungumzia kifo hicho, mke wa marehemu, Modesta Makaidi, alisema mumewe hakuwa na hali nzuri tangu juzi jambo lililowafanya wampeleke katika Zahanati ya Best kwa ajili ya matibabu.

“Juzi alikuwa amechoka choka tukalazimika kumpeleka katika Zahanati ya Best iliyoko wilayani Masasi ambapo alipumzishwa kuanzia saa tano asubuhi hadi saa 12 jioni aliporuhusiwa.

“Jana (juzi) alishinda nyumbani akiwa hajisikii vizuri kwani mwili wake haukuwa na nguvu kwani alishindwa hata kwenda kwenye kampeni zinazoendelea nchini.

“Leo (jana) asubuhi aliamka na kuwaita mawakala na kuanza kuwapanga huku akijiandaa kwenda kwenye kampeni, lakini  ilipofika saa tano hivi, nguvu zilianza kumwishia, akachoka na tukalazimika kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Nyangao iliyopo mkoani Lindi ambako alipoteza maisha,” alisema mke huyo wa marehemu.

Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyangao, Betram Makota, alisema Dk. Makaidi alifikishwa hospitalini hapo jana akiwa amepoteza fahamu.

“Tulipompima, vipimo vilionyesha alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu ndiyo maana alikuwa ameishiwa nguvu na hatimaye kupoteza maisha,” alisema Dk. Makota.

 

LOWASSA AMLILIA

Saa chache baada ya kifo hicho, mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa, alituma taarifa kwa vyombo vya habari na kusema alipokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko.

“Nimepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa NLD ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi.

“Mzee Makaidi alikuwa simba wa mabadiliko kwani pamoja na umri wake mkubwa, muda wote aliweza kuhimili vishindo vya mahasimu wa mabadiliko.

“Alipambana mpaka pumzi yake ya mwisho katika kuleta mabadiliko ya kisiasa ambayo ndiyo kiu ya Watanzania.

“Mzee Makaidi alikuwa mmoja wa nguzo imara katika Ukawa, hekima, busara na uaminifu wake ndivyo vilivyoufanya umoja wetu kuwa tumaini jipya na pekee kwa Watanzania.

“Amefariki siku 10 tu kabla ya kwenda kupiga kura. Nawaomba Watanzania tumuenzi shujaa huyu wa mabadiliko kwa kuwapatia kura wagombea wote wa Ukawa kuanzia udiwani hadi urais.

“Mzee Makaidi tunamuahidi kuendeleza bila kuchoka kazi aliyoiacha ya kuwaletea Watanzania mabadiliko ili waondokane na umasikini. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” alisema Lowassa.

 

WASIFU WAKE

Dk. Makaidi alizaliwa Aprili 20, mwaka 1941 wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara na alisoma Shule ya Msingi Namalenga, Masasi kati ya mwaka 1948 hadi 1952.

Baadaye alijiunga na Shule ya Kati (Middle School) Luatala kati ya mwaka 1953 hadi 1953.

Mwaka 1953, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph hadi mwaka 1956 alipohitimu kidato cha nne. Mwaka 1957 hadi 1958 alisoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Luhule iliyoko Uganda.

Mwaka 1973, alijiunga na Chuo Kikuu cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini alikosomea shahada ya kwanza ya uhandisi na alihitimu masomo hayo mwaka 1976.

Mwaka 1960 hadi 1962 alisomea shahada ya uzamili katika menejimenti ya utawala nchini Marekani.

 

KAZI

Dk. Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966 hadi 1973 akiwa kama mchambuzi kazi mkuu katika kitengo cha utumishi.

Kati ya mwaka 1974 na 1975, alirudi masomoni ambapo alijiunga na kuhitimu masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard nchini Marekani.

Alirejea nchini 1976 na kuendelea na kazi yake hadi 1985 alipoteuliwa kuwa mkurugenzi wa miundo na mishahara kwenye kamati iliyokuwa inashughulikia mashirika ya umma.

Akiwa anaendelea na kazi hiyo, mwaka 1977 alipata nafasi ya kwenda kusoma stashahada ya kuchakata taarifa za kielektroniki katika Chuo Kikuu cha Trinity nchini Ireland.

Mwaka 1985, alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii na mwaka huo huo alifukuzwa kazi na kuajiriwa katika kampuni binafsi ya Finwork Directory kama mkurugenzi mtendaji hadi 1992 alipoamua kuachana na kazi za kuajiriwa.

 

SIASA

Dk. Makaidi alianza kujihusisha na siasa mwaka 1992 akiwa Mwenyekiti wa NLD na mwaka 2005 katika uchaguzi mkuu,  aliteuliwa na chama chake kuwania urais.

Wakati huo, alikuwa miongoni mwa wagombea kumi wa vyama mbalimbali na alishika nafasi ya saba kwa kupata asilimia 0.19 ya kura zote za urais.

Mwaka 2010, alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge katika Jimbo la Masasi ambapo alishika nafasi ya tatu.

Mwaka 2014 alikuwa ni miongoni mwa watu waliochaguliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, na chama chake kilikuwa miongoni mwa vyama vilivyojitoa kwenye mchakato huo na hatimaye kuunda Ukawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles