30.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

MWENYEKITI TANDALE ADAIWA KUTAFUNA FEDHA

Na CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM


MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, amempa saa 24 Mwenyekiti wa Mtaa wa Sokoni, Murshida Diswela,  awe amejisalimisha polisi na kukabidhi fedha za wananchi zinazodaiwa kutafunwa.

Akizungumza na wananchi wa Tandale Dar es Salaam jana katika ufunguzi wa ziara yake ya siku 20, Hapi alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Mulilo, kuhakikisha anamkamata mwenyekiti huyo na awekwe ndani ili arejeshe fedha hizo vinginevyo hatua kali zitachukuliwa.

Hapi aliyasema hayo kwa sababu ya malalamiko yaliyotolewa na wananchi kuwa, wamechangishwa Sh 40,000 kila nyumba kwa muda mrefu lakini hadi sasa hawafahamu fedha hizo zilizodaiwa za ujenzi wa mfereji zilipokwenda.

Mjumbe wa nyumba 10, Asha Ally, alisema tangu wachange fedha hizo mwaka 2015 kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa Mto Ng’ombe, viongozi wao wametoweka na hawana majibu ya kuridhisha.

Kauli hiyo ilimfanya Hapi amuinue Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Athuman Mtoro ambaye alisema fedha hizo hafahamu zilipo na mwenye kujibu tuhuma hizo ni mwenyekiti wa Mtaa Diswela ambaye alizikusanya.

“Kwa kuwa mwenyekiti wa mtaa huo hayupo na ndiye mwenye fedha hizo, naagiza kamanda wa polisi amkamate ndani ya saa 24 fedha hizo ziwe zimerejeshwa,” alisema Hapi.

Pia alisema ana taarifa kuwa, baadhi ya watendaji wamekuwa wakitumia vibaya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa kuwaandikisha majina ya vijana ndio wapewe misaada huku wakiwaacha wenye mahitaji maalumu.

“Nina taarifa watendaji wengi wana majibu mabaya, hivyo wananchi kukosa uelewa mzuri wa taratibu za hospitali na sera zilizopo, ni vyema mkawapa watumishi wenu taratibu nzuri,” alisema Hapi.

Alisema tangu aingie madarakani katika wilaya hiyo, tayari amesikiliza migogoro 637 ya ardhi na kuipatia ufumbuzi.

Alisema ili kusikiliza kero ipasavyo za wananchi, ameamua kugawa kanda nne baada ya ziara na kutenga siku 16 kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi.

Alisema hadi sasa manispaa hiyo imetengeneza madawati 7,319, pia wametenga Sh bilioni 3.8 za vijana na wanawake.

Aliongeza kuwa katika kufanya wilaya hiyo inakuwa ya kisasa, tayari Soko la Tandale lipo katika mchakato wa ujenzi ambapo Sh milioni 100 zimetengwa na Sh bilioni  9 za ujenzi wa Soko la Magomeni ambalo litakuwa la ghorofa na upande wa chini maegesho ya magari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,509FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles