27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenyekiti mpya Bodi ya REA aanza kazi rasmi, asisitiza kuchapa kazi

Na Veronica Simba – REA

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Nishati Vijijini, Janeth Mbene ameanza kazi rasmi kwa kukutana na kuzungumza na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambapo amesisitiza uchapakazi, weledi, uadilifu na ushirikiano katika kazi.

Katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam leo, Februari 11, 2023 na kuhudhuriwa pia na Wajumbe wa Bodi, Mwenyekiti amehamasisha kufanya kazi kwa ufanisi ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa katika kuwasaidia wananchi hususan wa vijijini kupata maendeleo.

“Tujitahidi sana kufanya kazi vizuri, kwa weledi na kwa wakati huku tukisimamia maeneo ambayo tunapaswa kuyasimamia kwa karibu sana hasa wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali,” amesisitiza Mwenyekiti.

Akizungumza zaidi, Mbene ameeleza kuwa maendeleo ya kiuchumi yanategemea sana nishati za aina zote, hivyo akatoa hamasa kwa wafanyakazi wa REA kupitia Menejimenti kutumia vizuri rasilimali kidogo zinazopatikana ili tija yake ionekane.

Amesema REA ni Taasisi yenye umuhimu mkubwa kwa Taifa kutokana na mchango wake katika maendeleo hususani ya wananchi wa vijijini. “Na kwa hali hiyo hii kazi tuliyopewa siyo ndogo,” amesisitiza.

Zaidi, Mwenyekiti amewataka wote kuhakikisha wanafanya kazi inayoacha alama na kwa namna hiyo kuzitendea haki nafasi walizopewa kuwatumikia Watanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote wa REA, Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy amemhakikishia Mwenyekiti ushirikiano na kwamba watatekeleza yote aliyoyaagiza.

Awali, Wajumbe wa Menejimenti walipata fursa ya kujitambulisha kwa Mwenyekiti na kila mmoja kueleza majukumu yanayotekelezwa katika Idara/Kitengo anachosimamia.

Janeth Mbene aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Februari Mosi, 2023 na kutangazwa Februari 3, mwaka huu kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini baada ya Mtangulizi wake kumaliza muda wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles