MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Sangabuye, John Luhela, anatuhumiwa kukatisha masomo ya mwanafunzi kidato cha pili katika shule ya sekondari Sangabuye, Lucia Daudi, na kuishi naye kinyumba kwa mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika mtaa huo, Luhela alimuoa mwanafunzi huyo kwa kulipa mahari ya Sh 200,000 na kusababisha akatishe masomo yake mwaka jana.
Inasemekana hivi sasa mwanafunzi huyo ni mjamzito.
Mwandishi alifika nyumbani kwa Luhela ambaye alieleza kumfahamu Lucia kama mtu wake wa karibu.
Alisema wakati msichana huyo alikuwa amekwenda nyumbani kwa mama yake mzazi (mama wa Luhela) ambako alimwacha baada ya kumaliza msiba wa kaka yake.
Mama yake Luhela naye alisema Lucia alikuwapo hapo lakini aliondoka baada kumaliza kula chakula cha mchana na hakueleza alikoelekea.
Mama wa Lucia, Agness Kadirana, alipoulizwa alisema mwanae aliacha shule mwaka 2013 akidai kuwa shule imemchosha na kwamba alitaka ajifunze ufundi cherehani.
Alisema mara ya mwisho alimuaga kuwa alikuwa anakwenda Igoma wilayani Nyamagana kwa mdogo wake.
Kuhusu taarifa ya kupokea mahari kwa ajili ya kumuoza mwanae kwa mwenyekiti wa mtaa huo, Agness alikana madai hayo.
Alisema hajawahi kupokea fedha yoyote na hana lolote na akasisitiza kuwa hana lolote la kusema kuhusu ujauzito wa mtoto wake kwa sababu mwanae huyo ana baba yake.
Hata hivyo, Agness, mama mzazi wa Lucia na mwenyekiti wa mtaa wa Sangabuye, wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kirumba kwa uchunguzi wa tukio hilo.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sangabuye, Stephen Mhagama, alikiri binti huyo alikuwa mwanafunzi wa shule hiyo.
Mwalimu Mhagama alisema kwa sasa binti huyo angetakiwa kuwa kidato cha tatu lakini alianza utoro tangu Juni mwaka jana baada ya kumaliza muhula wa kwanza wa masomo.
“Nilijitahidi kufuatilia wanafunzi wote ambao hawahudhurii masomo kupitia mpango wa kukomesha utoro wa rejareja nikapata taarifa Lucia amewekwa kinyumba na kiongozi wa serikali ya mtaa wa Sangabuye. Ndiyo sababu hakufanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili.
“Kwa mujibu wa sheria za Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, mwanafunzi anapomaliza kidato cha nne suala la kuolewa linatakiwa kusubiri miaka miwili.
“Akiolewa mara tu baada ya kumaliza anakuwa bado ni mwanafunzi, nawaomba wananchi wasitumie hali ngumu ya uchumi wa familia za wanafunzi kuwarubuni,” alisema Mhagama.
Juhudi za mwandishi kumtafuta mwanafunzi huyo kwa kushirikiana na polisi wilayani Ilemela ziligonga mwamba.