33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenge wazindua miradi ya bilioni 12.2/- Ilala

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MIRADI sita yenye thamani ya Sh bilioni 12.2 imezinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa wilayani Ilala.

Mwenge huo uliingia Dar es Salaam Ijumaa iliyopita ukitokea Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na kuanza kukimbizwa katika Wilaya ya Ilala.

Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alisema kwa mwaka 2018/2019 walipanga kutekeleza miradi yenye thamani ya Sh bilioni 71.1 na kati ya fedha hizo Sh bilioni 22.3 ni mapato ya ndani na Sh bilioni 48.7 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu.

“Kati ya miradi itakayozinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi ipo ambayo imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi na mingine iko kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji,” alisema Mjema.

Miradi hiyo na sehemu ilipo kweye mabano ni kituo cha vijana cha ubunifu wa teknolojia mbalimbali na kilimo cha kisasa (Kata ya Kitunda), ujenzi wa hospitali ya wilaya (Kata ya Kivule), mradi wa maji wa Dawasa unaohusisha ujenzi wa tanki la zege la kuhifadhia maji lenye uwezo wa ujazo wa lita milioni 2 (Kata za Pugu Stesheni, Majohe, Buyuni, Chanika, Gongo la Mboto, Ukonga na Kipawa).

Mingine ni ujenzi wa hospitali binafsi ya Kitonka (Kata ya Ukonga) na choo cha mtoto wa kike katika Shule ya Msingi Ilala (Kata ya Ilala).

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mjema alisema wameanza kutoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uelewa waweze kutumia haki yao kikatiba kuchagua viongozi bora bila kushawishiwa. 

Awali akipokea mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, alisema miradi 35 yenye thamani ya Sh bilioni 123.6 itapitiwa wakati wa mbio hizo. 

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkongea Ali, aliipongeza Wilaya ya Ilala kwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo, lakini akawataka kuhakiki ubora wa vifaa vyote vya ujenzi kupitia mamlaka husika kabla havijapelekwa eneo la ujenzi.

“Tunahakiki umakini na thamani ya fedha inayotolewa ili kuepuka kumpendelea mtu, tunataka haki itendeke kwa kila mtu,” alisema.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles