28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenge wa Uhuru wapokelewa kwa shangwe Iramba

Na Seif Takaza, Iramba

Wananchi wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, wameupokea kwa furaha Mwenge wa Uhuru katika Kijiji cha Maluga, ukitokea Manispaa ya Singida. Mwenge huo utaanza safari ya urefu wa kilomita 68, ukipitia miradi saba muhimu katika wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, alikabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, ukitokea Singida Mjini. Mwenda aliahidi kuulinda na kuutunza Mwenge huo hadi atakapoukabidhi Wilaya ya Mkalama.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzarva, alitoa shukrani kwa kufika salama wilayani Iramba na kuwapongeza wananchi kwa kufuata falsafa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.

Pongezi hizo zilitolewa wakati Mzarva akiweka jiwe la msingi katika Kiwanda cha kukamua Mafuta ya Alizeti kijijini Kyengege. Alisema ni jukumu la Rais Dk. Samia kuboresha mazingira ya sekta binafsi ili wawekezaji waweze kufanya biashara kwa amani.

“Maelekezo yake ni kuhakikisha taasisi zote zinazohusika na biashara na uwekezaji zinakuwa rafiki ili kuvutia wawekezaji na kulinda usalama wa mitaji yao. Rais wetu anafanya haya kupitia falsafa yake ya ushirikishaji wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi,” alisema Mzarva.

Aidha, Mzarva alisisitiza kuwa wakulima wa zao la alizeti wamepata uhakika wa soko kupitia kiwanda hicho, hali inayowawezesha kulipa kodi na kupata kipato kikubwa. Alimpongeza mmiliki wa kiwanda hicho, Hamoud Adim, kwa kutoa ajira na huduma kwa wananchi.

Awali, mwakilishi wa mmiliki wa kiwanda, Yasini Mbolole, alisoma taarifa fupi mbele ya Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa, akisema mradi huo umegharimu shilingi milioni 95. Mbolole aliongeza kuwa mradi huo unamchango mkubwa katika kuwahudumia wananchi wa vijiji vya Makunda, Kyengege, Mugundu, Kitukutu na Ulemo.

Mbolole alifafanua kuwa wananchi wanaweza kuongeza thamani ya mazao yao na kupata soko la uhakika kwa wakulima wakubwa na wadogo. Mradi huo pia umechangia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wa maeneo hayo.

Mbio za Mwenge wa Uhuru zimefanikiwa kutembelea, kuona, kuweka mawe ya msingi, na kuizindua miradi saba yenye thamani ya Sh bilioni 5.084, fedha zilizotolewa na serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles