25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 27, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mwekezaji wa shamba la VASSO Moshi adai kufukuzwa isivyo Halali

N Safina Sarwatt, Kilimanjaro

wekezaji wa shamba la VASSO lililopo Kijiji cha Dakau, Wilaya ya Moshi Vijijini, Fons Nijenhuis (73), raia wa Uholanzi, amedai kufukuzwa kwa nguvu na watu wasiojulikana, huku kundi kubwa likivamia makazi yake, kufanya uharibifu wa mali, na kupora fedha. 

Kwa mujibu wa Nijenhuis, uvamizi huo ulisababisha mauaji ya farasi wake wawili na uporaji wa Euro 10,000, huku mke wake akijeruhiwa vibaya. Ameiomba Serikali kuingilia kati, akidai kuwa hakujulishwa rasmi wala kupewa hati ya kusudio la kufukuzwa shambani hapo. 

Mwekezaji huyo alisaini mkataba wa uwekezaji wa miaka 30 na Chama cha Ushirika wa Mazao cha Kibosho Kati mwaka 2003, na baadaye akaurefusha hadi mwaka 2058. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Nijenhuis alilalamika vikali akisema: 

“Wamenifukuza kama takataka, huu ni unyama. Haya mambo yanafanyika Zimbabwe, siyo Tanzania. Naomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati, mimi siodoki hapa mpaka wanirudishie shamba langu,” alisema kwa uchungu. 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, amesema Serikali inafuatilia suala hilo na itatoa taarifa rasmi. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Kibosho Kati, Fabian Mallya, amekanusha kuhusika na kufukuzwa kwa mwekezaji huyo katika shamba lenye ekari 181.13. 

Wakulima Wanadai Rejesho la Ekari 37

Wakati huohuo, zaidi ya wanachama 70 wa Chama cha Ushirika wa Mazao (AMCOS) wanadai kurejeshewa ekari 37 ambazo wanadai zimeuzwa kwa watu binafsi kinyume na makubaliano. Wanachama hao wanasema shamba hilo, sehemu ya shamba la Antippi, lilipaswa kutumika kwa upanuzi wa shule za msingi Kidachini, Masoka, na Ngirinyi, pamoja na taasisi za kijamii kama Kanisa Katoliki Kirima, Msikiti wa Kirima, na ujenzi wa kituo cha afya. 

Katika barua yao ya hivi karibuni kwa mamlaka husika, wanachama hao walisema: 

“Sisi wanachama wa Kirima Boro AMCOS LTD, kwa kauli moja, tumeafikiana kuwa ekari 37 zilizotengwa kwa ajili ya taasisi zirejeshwe kwa Antippi Estate ili tumkabidhi mwekezaji VASSO Agroventure LTD,” inasema sehemu ya barua hiyo. 

Mmoja wa viongozi wa zamani wa kisiasa, ambaye pia ni mdau wa maendeleo wa Kata ya Kibosho Kirima, ameungana na wanachama hao kutaka ardhi yao irejeshwe. 

Katika barua yake ya Agosti 28, 2023, kwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, mdau huyo aliomba hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika na kuporwa kwa ekari hizo, akisema: 

“Ekari 37 za shamba la Antippi Estate zilipaswa kutumiwa kwa taasisi za kijamii, lakini zimeporwa na kumilikishwa kwa watu wasio walengwa. Serikali ichukue hatua za kurejesha haki.” 

Mamlaka ya ushirika yapinga taratibu zilizotumika

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, Jacqueline Senzigha, amesema hana taarifa rasmi za malalamiko hayo, lakini amekiri kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika utoaji wa ardhi hiyo. 

“Kabla ya shamba hilo kutolewa, mkutano mkuu wa wanachama ulipaswa kufanyika na mhutasari wake kuwasilishwa ofisini kwetu kisha kwa Mrajis kwa maamuzi ya mwisho. Jambo hilo halikufanyika,” amesema Senzigha. 

Serikali imeahidi kufuatilia suala hilo kwa karibu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote zinazohusika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
596,000SubscribersSubscribe

Latest Articles