26.8 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Mwarobaini ajali ni kubadili sheria

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SERIKALI  imeelezwa ili kupunguza ajali barabarani inatakiwa ikamilishe mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 ambayo inatarajia kugusa maeneo yote yenye upungufu na yanachangia kusababisha ajali.

Hayo yalielezwa jana bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Musa Zungu wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha Januari mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

Zungu alisema pamoja na jitihada za Serikali katika kupunguza ajali za barabarani, kamati imebaini kuwa lipo ongezeko la watumiaji wa barabara wasiotii sheria za usalama barabarani kama vile madereva wa bodaboda ambao wanaendelea kusababisha ajali.

“Kamati inaamini kuwa ili kufanikiwa zaidi katika kudhibiti ajali barabani ni muhimu ikamilishe mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ambayo inatarajia kugusa maeneo yote yenye upungufu ambayo yanachangia kusababisha ajali,” alisema.

Pia kamati ilishauri Serikali kupeleka watumishi zaidi ambao wana taaluma ya masuala ya uchumi ili kuziwezesha balozi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

“Aidha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii itengeneze mkakati thabiti wa kuziwezesha balozi zetu kutambua utalii.

“Mkakati huu ni pamoja na kutenga na kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kutangaza utalii nje ya nchi pamoja na kutumia watu mashuhuri waliowahi kutembelea vivutio vya utalii nchini,” alisema.

Kamati hiyo iliishauri Serikali ione umuhimu wa kutumia mikopo ya muda mrefu, lakini yenye tija katika kuendeleza viwanja vya balozi zake ambazo zimetelekezwa kama London, Oman na Nairobi.

“Hii itasaidia Serikali kuokoa fedha nyingi za walipakodi zinazotumika kwa ajili ya kodi za pango na fedha hizo kuendelezwa katika miradi mingi ya maendeleo,” alisema.

Pia Jeshi la Magereza liandae mkakati madhubuti wa kujitosheleza kichakula ikiwa ni pamoja na kutumia rasilimali za ardhi, nguvu kazi na zana za kilimo walizonazo katika kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya magerezani.

“Serikali itenge fedha kwa ajili ya kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika makambi na vyuo vya jeshi ili kuondoa migogoro ya ardhi kati ya majeshi na wananchi,” alisema Zungu.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,263FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles