23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanza yatambulisha mradi wa huduma endelevu za Maji

Na Clara Matimo, Mwanza

Jumla ya vituo 82 vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika halmashauri sita kati ya nane zilizopo mkoani Mwanza zitanufaika na mradi wa huduma endelevu za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni sita.

Mradi huo wa 2022/23  unatekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR TAMISEMI).

Baadhi ya watendaji waliohudhuria uzinduzi wa mradi  wa huduma endelevu za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni sita.

Hayo yamebainishwa leo Februari 11, 2023 jijini Mwanza na Kaimu Afisa Afya wa mkoa humo, Pascal Malimani wakati akitambulisha mradi huo ambao utatekelezwa katika halmashauri za  Buchosa, Misungwi, Magu, Sengerema, Ukerewe na Kwimba.

Malimani amesema mradi huo unaotarajiwa kukamilika Juni 30, 2023 unamalengo mbalimbali ikiwemo kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika ngazi ya kaya pamoja na kuhimiza wananchi tabia ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

“Malengo mengine ya mradi huu ni kuboresha miundombinu ya maji na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri, kuongeza idadi ya vijiji ambavyo vimefikia daraja la juu la usafi kwa kuhakikisha kaya zote zinakuwa na vyoo bora na kuondoa kabisa tabia ya kujisaidia hovyo,” amesema Malimani.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amewataka watendaji wanaosimamia mradi huo kuhakikisha wanatembelea maeneo yaliyolengwa ili kupata taarifa na takwimu sahihi za usafi wa mazingira katika kaya na taasisi kwa kila robo ya mwaka ili kubaini mapema changamoto zilizopo na kuendelea kuhamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo bora.

“Hakikisheni mnawahamasisha wananchi  kujenga vyoo bora pamoja na matumizi ya maji tiririka na sabuni ili kunusuru wananchi dhidi ya magonjwa ya kuhara maana takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu 100,000 waliugua magonjwa ya kuharisha mwaka 2022 ambapo kati yao  zaidi ya asilimia 70 walikuwa ni watoto wenye umri  chini ya miaka mitano ni wajibu wetu kuwalinda watoto hao,”amesema Malima.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Thomas Rutachunzibwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa huo, Claudia Kaluli amesema wamebaini kwamba wananchi wengi wanatumia vyoo ingawa hawafahamu ubora wa vyoo jambo ambalo linaweza kuzidisha kuenea kwa magonjwa ya kuhara hivyo mradi huo utasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo ya mradi kunufaika kwa kupewa elimu ya jinsi ya kujenga vyoo bora.

Uzinduzi wa mradi huo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Baklandya Elikana,  wakuu wa Wilaya ambazo zitatekeleza mradi huo, wakurugenzi, maafisa afya na makatibu tawala  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles