Na Clara Matimo, Mwanza
Jumla ya vituo 82 vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika halmashauri sita kati ya nane zilizopo mkoani Mwanza zitanufaika na mradi wa huduma endelevu za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni sita.
Mradi huo wa 2022/23 unatekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR TAMISEMI).
Hayo yamebainishwa leo Februari 11, 2023 jijini Mwanza na Kaimu Afisa Afya wa mkoa humo, Pascal Malimani wakati akitambulisha mradi huo ambao utatekelezwa katika halmashauri za Buchosa, Misungwi, Magu, Sengerema, Ukerewe na Kwimba.
Malimani amesema mradi huo unaotarajiwa kukamilika Juni 30, 2023 unamalengo mbalimbali ikiwemo kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika ngazi ya kaya pamoja na kuhimiza wananchi tabia ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
“Malengo mengine ya mradi huu ni kuboresha miundombinu ya maji na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri, kuongeza idadi ya vijiji ambavyo vimefikia daraja la juu la usafi kwa kuhakikisha kaya zote zinakuwa na vyoo bora na kuondoa kabisa tabia ya kujisaidia hovyo,” amesema Malimani.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amewataka watendaji wanaosimamia mradi huo kuhakikisha wanatembelea maeneo yaliyolengwa ili kupata taarifa na takwimu sahihi za usafi wa mazingira katika kaya na taasisi kwa kila robo ya mwaka ili kubaini mapema changamoto zilizopo na kuendelea kuhamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo bora.
“Hakikisheni mnawahamasisha wananchi kujenga vyoo bora pamoja na matumizi ya maji tiririka na sabuni ili kunusuru wananchi dhidi ya magonjwa ya kuhara maana takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu 100,000 waliugua magonjwa ya kuharisha mwaka 2022 ambapo kati yao zaidi ya asilimia 70 walikuwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni wajibu wetu kuwalinda watoto hao,”amesema Malima.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Thomas Rutachunzibwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa huo, Claudia Kaluli amesema wamebaini kwamba wananchi wengi wanatumia vyoo ingawa hawafahamu ubora wa vyoo jambo ambalo linaweza kuzidisha kuenea kwa magonjwa ya kuhara hivyo mradi huo utasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo ya mradi kunufaika kwa kupewa elimu ya jinsi ya kujenga vyoo bora.
Uzinduzi wa mradi huo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Baklandya Elikana, wakuu wa Wilaya ambazo zitatekeleza mradi huo, wakurugenzi, maafisa afya na makatibu tawala