33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Mwanza yaanza mchakato wa kutekeleza mfumo wa usafiri wa dharura kwa wajawazito

*Unahusu pia mama waliojifungua na watoto wachanga

Na Clara Matimo

Katika kuhakikisha wanawake wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga wanaepuka vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kufika  mapema kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, serikali imeanza mchakatto wa kutekeleza mfumo wa upatikanaji wa usafiri wa dharura(M-Mama) mkoani Mwanza.

Baadhi ya washiriki wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe mkoani Mwanza na utambulisho wa mfumo wa M-Mama kwa wanawake wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Adama Malima(hayupo pichani).

Ikumbukwe kwamba mfumo huo ulizinduliwa rasmi Aprili, 6, 2022  na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kisha akaagiza utekelezwe nchi nzima uliishaanza kufanya kazi miaka kadhaa iliyopita katika maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa na idadi kubwa ya vivyo vya wanawake wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga kwa ufadhili wa wadau wa maendeleo ambao ni Vodacom Foundation, Touch Foundation na Pathfinder International kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na OR- Tamisemi.

Akizungumza jijini Mwanza hivi karibuni wakati akitambulisha mfumo huo wa M-Mama, Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto kutoka OR Tamisemi, Dk. Yahaya Hussein alisema utaongeza wigo wa upatikanaji wa usafiri wa dharura kwa kuwa utahusisha pia magari ya wanajamii ambao watakuwa wamepewa mafunzo maalum kisha kusajiliwa ili yatumike kama gari la kubeba wagonjwa likiwa halipo kituoni kutokana na sababu yoyote ikiwemo kuharibika au kuwa limepeleka mgonjwa katika kituo kingine.

“Tunamagari yetu ya serikali ya kubeba wagonjwa ambayo ndiyo huwa tunayatumia dharura zinapotokea kwa wagonjwa wote, mfumo wa M-Mama yaani Mobile –Mama utalenga kusafirisha mama mjamzito, mwanamke aliyejifungua ndani ya siku 42 au mtoto mchanga kutoka siku 0 hadi 28 anayehitaji huduma ya ziada kutoka kituo kimoja kwenda ngazi ya juu, ieleweke kwamba mfumo huo wa usafiri hautahusika na wagonjwa waliopo majumbani.

Dk. Hussein alisema mfumo huo utakuwa na faida kadhaa ikiwemo kuwa na utaratibu rasmi utakaowawezesha watendaji wa afya kuomba gari la wagonjwa inapotokea dharura kwa kupiga namba 115 kwenye hospitali za rufaa za mikoa badala ya kumpigia mganga mkuu wa wilaya au mkoa ambazo zitapokelewa na wataalamu wenye vishikwambi ambavyo vitawaelekeza gari lililosajiriwa linalopatikana karibu katika kituo hicho.

“Faida nyingine ni kwamba wahuduma wa afya watakuwa na uhakika wa wanapompeleka mgonjwa kama ni kituo cha kati au cha juu na wakati mteja anachukuliwa kutoka kituo cha ngazi ya chini kwenda kituo cha ngazi ya juu taarifa zitakuwa zimeishatumwa kwenye kituo atakachopokelewa hivyo watendaji wetu watakaompokea watakuwa wameishajiandaa kwa hiyo rufaa inapofika watatoa huduma inayostahili kwa mgonjwa,”alisema Dk. Hussin.

Mkuu wa mfumo wa M-Mama Tanzania, Rahma Bajun kutoka Vodacom Foundation alisema wamekuwa wakishiriki katika mambo mbalimbali ya kijamii, kitaifa na  kidunia hivyo waliamua kushiriki kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa sababu wanaamini hakuna mwanamke anayestahili kufa wakati analeta uhai mwingine duniani pia hakuna mtoto anayestahili kupoteza maisha pale ambapo kifo chake kingeweza kuzuiliwa akazaliwa salama.

“Tulibaini vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vinachangiwa na ucheleweshwaji kwenye maeneo makubwa matatu, kuchelewa kufanya maamuzi kwenda kupata huduma za afya aidha kwa kukosa pesa au uelewa endapo ataona hali ya hatari, ucheleweshwaji wa usafiri kutoka nyumbani kwenda  kituo cha afya au kituo cha afya kupelekwa kituo cha ngazi ya juu pale anapopata rufaa.

“Eneo la tatu ni upatikanaji wa usafiri,  mama anapofika kwenye kituo cha afya kupata huduma kama tunavyofahamu Tanzania bado tunachangamoto ya kila kituo na wilaya kuwa na gari la wagonjwa hivyo tukaona tusaidie kuweka mfumo ambao utawezesha hata madereva wa kijamii washiriki kusafirisha mama na mtoto kumuwahisha kituo cha ngazi ya juu,”ameeleza Bajun ambaye amefafanua kwamba jukumu lao ni kuhakikisha mfumo huo unafika wilaya zote nchini.

Kwa mujibu wa Bajun hadi sasa wameishasafirisha wagonjwa zaidi ya 16,000  katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Tanga, Zanzibar na Dodoma ambako mfumo wa M-Mama unatekelezwa hivi sasa wanaendelea na mchakato kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Simiyu , Mwanza na Shinyanga muda si mrefu mfumo huo utaanza kufanya kazi huko.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amewataka watumishi wa afya ambao watapata mafunzo ili kuutekeleza mfumo huo kuwasiliana na wenzao wa mikoa mingine ambayo imeishafanyiwa majaribio wawape uzoefu lengo ni kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi mkoani humo.

Afisa Lishe wa Mkoa wa Mwanza, Sophia Lazaro, (aliyesimama) akitoa taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe mkoani humo kuanzia Julai hadi Desemba 2022 kwenye  kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe.

Malima alitoa  wito kwa wanawake wajawazito mkoani humo kufika mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya wanapobaini changamoto yoyote iwe rahisi kuhudumiwa hata kwa kufikishwa katika vituo vya ngazi ya juu endapo watakuwa na shida ili kujiepusha na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Utambulisho wa mfumo wa M-Mama mkoani Mwanza uliambatana na tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2022 ambapo Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kutenga fedha za lishe kwa wakati ili kupunguza tatizo la utapiamlo na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,079FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles