24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Mwanyika aachiwa baada kumalizana na DPP

 KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewaachia huru aliyekuwa Rais wa Migodi ya Pangea North Mara, Exploration na Bulyanhulu, Deogratius Mwanyika na wenzake wawili, baada ya kulipa fidia ya Sh bilioni 1.5 na faini Sh milioni 4.5.

Hukumu hiyo, ilitolewa na mahakama jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya, baada ya washtakiwa kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kumaliza kesi hiyo.

Washtakiwa hao, endapo wangeshindwa kulipa faini ya Sh milioni 4.5 ,waliamuliwa kwenda jela kila kila mmoja miezi minne.

Washtakiwa ambao wamekaa gerezani zaidi ya siku 526, waliondolewa mashtaka yote 38 na kubakiwa na shtaka moja la kukwepa kulipa kodi.

Mbali na Mwanyika, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ni Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu Alex Lugendo, Mkurugenzi Mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku, Assa Mwaipopo, Kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Kabla ya makubaliano, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya Dola za Marekani milioni 112.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili 11, mwaka 2008 na Juni 30, mwaka 2007 sehemu tofauti ya jiji la Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga, Tarime mkoani Mara, Biharamulo mkoani Kagera na maeneo ambayo yapo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maeneo mengine ambayo washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo, ni katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na Uingereza.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Isaya baada ya washtakiwa kukiri shtaka moja la kukwepa kodi aliwatia hatiani na kuwahumu kila mmoja kulipa faini ya Sh milioni 1.5 ambapo wote watalipa Sh milioni 4.5 na wakishindwa kufanya hivyo kila mmoja ataenda jela miezi minne.

Pia mahakama hiyo, imewaamuru kulipa fidia ya Sh bilioni 1.5 ambapo fedha hizo pamoja na faini zote zimelipwa kama walivyokubaliana.

Hakimu Isaya aliwasisitiza washtakiwa kutimiza makubaliano waliyofikia na DPP .

Washtakiwa wote wameachiwa huru, baada ya kulipa faini na fidia. Kabla ya kufutiwa mashtaka walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama , mashtaka saba ya kughushi , mashtaka 17 ya Utakatishaji wa fedha, kuwasilisha nyaraka za uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzanian (TRA), shtaka moja, kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka nane ya kukwepa kodi na shtaka moja la kutoa rushwa.

Pia mshtakiwa Mwanyika na Lugendo, wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.

Washtakwa hao, wanadaiwa kutoa tamko la uongo kwa Kamishna Jenerali wa TRA Biharamulo kwa nia ya kukwepa kulipa kodi ya wa Dola za Marekani 9,309,600 ambayo ilikuwa ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

Mshtakiwa Mwanyika na Lugendo, wanadaiwa kati ya Desemba,2009 na Julai 31, 2018 maeneo tofauti ndani na nje ya nchi ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha Dola za Marekani 374,243,943,45, huku wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

 Pia washtakiwa wanadaiwa kati ya Novemba 2, 2012 na Novemba 27, 2015 mkoani Shinyanga walitoa rushwa ya Sh 718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles