23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanri ‘kufyekelea’ mbali majosho mabovu

Na TIGANYA VINCENT TABORA

SERIKALI mkoani Tabora imetoa mwezi mmoja kwa halmashauri zake zote kuhakikisha majosho mabovu ya kuogeshea ng’ombe yanakarabatiwa na kuanza kufanyakazi ili kuwasaidia wafugaji kuwa na sehemu ya kupeleka mifugo yao kwa ajili ya kuikinga na maradhi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, wakati akizindua wiki ya uogeshaji ng’ombe kwa Kanda ya Magharibi katika Josho la Itetemia Manisapaa ya Tabora.

Alisema haiwezekani ng’ombe waendelee kufa kwa magonjwa mbalimbali wakati Serikali imenunua dawa aina ya Paranex na kuzisambaza maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kukabiliana na kupe, ndorobo na mbu waenezao ndigana kali ndigana baridi, mkojo mwekundu, homa ya bonde la ufa na maji moyo.

Mwanri alisema ni lazima majosho yote ambayo yamekufa yafufuliwe na yaanze mara moja kutoa huduma kwa wafugaji ili waweze kuwa na uzalishaji wenye tija.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ustawi wa wanyama na hatimaye kuongeza uzalishaji  na kupunguza vifo vya wanyama vinavyotokana na magonjwa yaenezwayo na kupe na ndorobo.

Naye Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Mifugo Kanda ya Magharibi Dk. Shabani Tozzo, alisema jumla ya lita 750 za dawa ya Paranex imepokelewa kwa ajili ya mikoa ya Tabora na Kigoma kwa ajili ya kugawia halmashauri zote ili zisaidie kukabiliana na kupe na ndorobo.

Alizitaka halmashauri zote kuhakikisha zinasimamia uogeshaji wa mifugo ili kuikinga na vifo vinavyosababishwa na magonjwa yanayoenezwa na kupe na ndorobo.

Dk. Tozzo alisema Kanda ya Magharibi (Tabora na Kigoma) ina jumla ya ng’ombe milioni 3.1, mbuzi milioni 1.4, kondoo zaidi ya laki 4, kuku milioni 5.5, nguruwe zaidi ya laki 1 na punda zaidi ya laki 1.

Alisema kanda hiyo ina jumla ya majosho 189 kati ya hayo mazima ni 63 sawa na asilimi 33 ya yote aliongeza kwa Mkoa wa Tabora una jumla ya majosho 111 ambapo mazima ni 18 sawa na asilimia 16.

Akisoma risala ya Chama cha Wafugaji Kikundi cha Ng’ombe Sabho Kata ya Itetemia, Makungu Kitula aliomba Serikali kuwaondoa watu waliovamia njia za kupitisha ng’ombe na kuwasababishia usumbufu wakati wa kupeleka mifugo yao mnadani Ipuli.

Aliomba pia Serikali iwasaidie kuwachimbia Bwawa kwa ajili ya kunyeshea mifugo yao ambayo imekuwa ikipata taabu wakati wa ukame. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles