ALIYEKUWA Waziri katika ofisi ya Rais, Kazi Maalum, Profesa Mark Mwandosya ameongoza mamia ya wananchi wa Wilaya ya Kyela, wakati wa ibada ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Athur Mwaitenda (79) aliyefariki dunia jijini Dar es Salaam juzi kwa ugonjwa wa kansa ya tezi dume.
Profesa Mwandosya aliitaka jamii nchini kuzisaidia familia za wafiwa pindi wazazi au walezi wao wanapofariki ili kujenga misingi ya upendo unaompendeza Mungu.
Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Kyela Mbeya na Profesa Mwandosya wakati wa ibada ya kumuaga marehemu Mwaitenda (79) aliyefariki dunia jijini Dar es Salaam kwa ugonjwa wa kansa ya tezi dume.
Mwandosya alisema Watanzania wanatakiwa tujenge misingi ya kutunza familia za wafiwa kwa kuwapa misaada ya hali na mali ukiwemo ushauri na si kufanya mashindano ya nani katoa rambirambi kubwa.
Alisema Mwaitenda wakati wa uhai wake ndiye aliyefanikisha mafanikio yake kutokana na marehemu baba yake Mzee Mwandosya kumkabidhi, akihitaji asaidiwe ambapo DCI, alimlea pamoja na kumfundisha kazi kama mwanae na kufanikiwa kuwa kiongozi mkubwa wa Taifa.
“Kutokana na Mzee Mwaitenda kunilea mimi kama mwanae, nitachukua jukumu la kuwa mwangalizi wa familia hii japo kuwa watoto sita wa familia hii wengi wao wanaishi nchini Marekani, pia napenda kutumia kitabu cha Zaburi 23 kikizungumzia kuhusu wajibu wa kifo ambapo kifo cha mzee huyu ni sherehe,’’alisema Mwandosya.