Kulwa Mzee -Dar es salaam
MWANDISHI wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera (39), anayekabiliwa na mashtaka matatu, likiwamo la kutakatisha zaidi ya Sh milioni 173, ataendelea kusota rumande hadi Agosti 30, kesi yake itakapotajwa.
Kabendera ambaye aliingia Gereza la Segerea wiki mbili zilizopita, jana kesi yake ilitajwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Mmbando baada ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile anayesikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kesi ilikuwa inatajwa, upelelezi haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 30, kwa kutajwa na mshtakiwa ataendelea kuwa rumande.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika shtaka la kwanza, kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019, maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kabendera na wengine ambao hawapo mahakamani, anadaiwa alitoa msaada kwenye genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha.
Katika shtaka la pili la kukwepa kodi, inadaiwa kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam bila sababu za msingi, mshtakiwa alikwepa kulipa kodi Sh 173,247,047.02 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, inadaiwa katika tarehe hizo mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zimetokana na zao la kusaidia genge la uhalifu na kukwepa kodi.