25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MWANDISHI ALIYEPIGWA NA POLISI ASEMA AMEFUNGULIWA KESI

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MWANDISHI Silas Mbise, anayeonekana katika video fupi iliyosambaa mitandao ya kijamii akishambuliwa na askari wa Jeshi la Polisi kwa mateke na ngumi, amefunguliwa kesi kwa kosa la kutaka kupigana na askari.

Pamoja na kwamba Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Lukula amekana taarifa hizo, Mbise mwenyewe ambaye alisema bado ana maumivu sehemu za mgongoni na kichwani kutokana na kipigo hicho, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa amefunguliwa kesi hiyo katika Kituo cha Polisi Chang’ombe kilichopo Temeke, Dar es Salaam.

“Nilikuwa nimeenda kufuatilia PF3, lakini nilipofika nikaambiwa nimefunguliwa jalada na nina kesi ya kutaka kupigana na polisi, nikaambiwa niandikishe maelezo yangu, nikafanya hivyo na meneja wa kituo chetu cha redio ndiye aliyenidhamini…tumeambiwa turudi tena siku ya Jumatatu,” alisema.

Mbise anayefanya kazi Wapo Radio, alisema kwa sasa suala hilo lipo chini ya meneja wa kituo chake cha kazi aliyejulikana kwa jina la Elibariki.

MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na Elibariki ambaye alikiri Mbise kufunguliwa jalada katika Kituo cha Chang’ombe.

“Tunahitaji haki itendeke, hatujafurahishwa, sisi na Jeshi la Polisi tunafanya kazi kwa kushirikiana, na Mbise mwenyewe suala hili alilisamehe, lakini kilichozua taharuki ni ile video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, tuna taarifa polisi hili suala wanalishughulikia, tunatamani hili suala liishe,” alisema Elibariki.

Alipotafutwa Kamanda Lukula alijibu kwa kifupi; “hapana si kweli” na kisha akakata simu.

Tukio la kupigwa kwa Mbise ambalo lilitokea Agosti 8 wakati wa mchezo baina ya timu ya Simba na Asante Kotoko ya Ghana walipokuwa wakiadhimisha Siku ya Simba (Simba Day), lilijulikana zaidi juzi kupitia video fupi iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Video inayoonyesha tukio la Mbise, imeibua hasira katika makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii ya wanataaluma ya habari na wale wa masuala ya haki za binadamu.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=RvZ9GXRivfg[/embedyt]

Tayari Baraza la Habari (MCT), Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamelitaka jeshi hilo kuwachukulia hatua kali polisi wote waliohusika katika kitendo hicho.

Video hiyo inamwonyesha Mbise akishambuliwa na askari wanne waliokuwa na silaha za moto na virungu, ambao walikuwa wakimpiga kwa vibao na mateke kwenye mbavu na kichwani, huku akiwa amelazwa chini na hana shati.

Kilichozua taharuki zaidi na hasa kwenye tasnia ya habari, ni kwamba tukio hilo limetokea wakati wiki ikiwa haijamalizika tangu mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma, akumbane na kipigo cha polisi akiwa anatekeleza majukumu yake huko Tarime mkoani Mara na kisha  kumpa tuhuma za kufanya maandamano yasiyo na kibali.

Akielezea tukio hilo na video inayosambaa katika mitandao ya kijamii, Mbise alisema yeye na waandishi wengine wa vyombo mbalimbali vya habari, walikuwa wanaelekea katika chumba cha mkutano, na walipofika katika mlango wa kungilia wakakuta umefungwa.

Alisema wakati wanasubiri, alifika askari mmoja aliyekuwa amevalia nguo za kiraia akiwa ameshika ‘radio call’ na kuwataka waondoke, huku akiwasukuma.

Mbise alipohoji kitendo hicho na kumtaka askari hiyo atumie taaluma yake, askari mwingine aliyekuwa amevalia sare aliingilia kati, akamkwida na kuanza kumpiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles