Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia kesi Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister Bitaho (54), ambaye alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo ya kuishi na kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa baada ya Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Method Kagoma, kuiomba mahakama kumfutia kesi hiyo chini ya kifungu cha 98(a)cha sharia ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Hata hivyo baada ya mshtakiwa huyo kuachiwa huru, alikamatwa tena na yupo Idara ya Uhamiaji kwa ajili kwa mahojiano.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay alimsomea mashtaka mshtakiwa huyo na kudai kuwa Mei 19, mwaka huu katika maeneo ya Kinondoni kwenye Ofisi ya Uhamiaji, Bitaho akiwa raia wa Burundi alikutwa akiwa nchini bila ya kuwa na kibali cha mkazi.
Alidai kuwa, siku hiyo mshtakiwa huyo alikutwa akifanya kazi kama mwanasheria Mkuu wa TBS bila ya kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya kazi hapa nchini.
Alidai kuwa, Julai 6 mwaka 2011 katika Ofisi ya Uhamiaji ya Dar es Salaam iliyopo wilaya ya Ilala, mshtakiwa huyo akiwa raia wa Burundi alitoa taarifa za uongo kuhusu maelezo yake binafsi wakati akijaza fomu ya kuomba hati ya kusafiria namba CT (5)(Ai).
Wakili Mlay aliieleza mahakama hiyo kuwa, kitendo hicho cha kutoa taarifa za uongo kilimuwezesha mshtakiwa huyo kupata hati ya kusafiria ya Tanzania yenye namba AB 474856 huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka huku upande wa jamhuri ukidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.