33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanamwema Shein apigia chapuo afya bora

Mwandishi wetu -Zanzibar

MKE wa Rais wa Zanzibar, Mwanamwema Shein amesema kwa kuzingatia umuhimu wa wananchi kuwa na afya bora, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele katika sekta ya Afya, kwa kuimarisha huduma mbali mbali .

Hayo aliyasema juzi katika uzinduzi wa huduma za upimaji afya kwa wazee wanaoishi katika nyumba za wazee Sebleni na Welezo, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano Sebleni, mjini hapa.

Timu ya madaktari bingwa kutoka Jamuhuri ya Watu wa China, wakishirikiana na madaktari wazalendo wameendesha zoezi la upimaji wa Afya kwa wazee wanaoishi katika nyumba hizo na kutoa huduma za uchunguzi, dawa na ushauri.

Alisema ili kufanikisha dhamira hiyo, Serikali imechukuwa hatua mbali mbali, ikiwa pamoja na kuimarisha miundombinu, kununua vifaa vya kisasa vya  uchunguzi, kuongeza bajeti ya dawa, kuongeza madaktari pamoja na kusomesha vijana wake ndani na nje ya nchi.

Alisema hivi sasa huduma za za Afya katika hospitali na vituo vya Afya kote nchini zimeimarika  na kutolewa bure , ikiwa ni hatua ya kufanikisha malengo ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu mzee Abeid Amani Karume.

Alieleza kuwa hatua ya  washirika wa maendeleo, ikiwemo Jamuhuri ya Watu wa China, kuunga mkono juhudi hizo kwa wataalamu wake kupima afya za wazee hapa nchini, ni jambo la kutia moyo na linalopasa kupongezwa.

“Kuwapima afya wazee wetu ni kuendeleza jitihada za kuwaenzi na kuwahudumia wazee wetu, hakika wazee hawa  walifanya kazi ya kutulea na kuijenga nchi yetu, hii ni kuonyesha tunawathamini, tunawajali na tunawapenda,” alisema.

Aliwataka wazee hao kuitumia vyema fursa waliyoipata na kutoa ushirikiano kwa wataalamu hao, ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Aidha,  alitoa wito kwa wazazi na walezi kote nchini kusimamia vyema malezi ya watoto wao kwa kuzingatia maadili mema, utamaduni  na silka za Wazanzibari, ili hatiame waweze kuwa raia wema.

Mama Mwanamwema alisitiza haja ya kuwahimiza watoto kuzingatia masomo yao ya skuli na madrasa pamoja na kuwafuatilia nyendo zao ili kuwaepusha na vitendo viovu, udhalilishaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Alitoa shukrani kwa timu hiyo ya madaktari kwa mara ya pili kukubali kutoa huduma za upimaji wa afya, hatua aliyobainisha inaonyesha mapenzi makubwa na urafiki uliopo kati ya wananchi wa China na Zanzibar.

Aidha, mama Mwanamwema alitowa ombi maalum kwa Ubalozi mdogo wa China uliopo Zanzibar akiomba huduma hizo zifikishwa kisiwa Pemba kwa ili wazee wanaoishi katika nyumba za wazee Limbani, nao waweze kufaidika.

Pia alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutimiza miaka tisa ya uongozi wake na kubainisha maendeleeo makubwa ya kiuchumi na  kijamii yaliofikiwa.

Awali Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Asha Suleiman Idd, aliwashukuru madaktri hao kwa moyo wao wa kujitolea na kuona umuhimu wa kuwaenzi na kuwahudumia wazee wa Zanzibar.

Naye, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, wazee, wanawake na watoto, Moudline Castico alipongeza juhudi endelevu za Mama Mwanamwema na Mama Asha Suleiman , ambapo kwa nyakati tofauti wamekuwa mstari wa mbele kutoa misada mbali mbali ya kijamii kwa wazee na watoto wanaolelewa katika nyumba za Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles