24.6 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

MWANAMKE ANAYEWANIA REKODI YA DUNIA YA MIGUU MIREFU

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI,

MAMA huyu wa watoto wawili, Caroline Arthur anapigania kuingia kwenye Kitabu cha Rekodi za Dunia, yaani Guiness Book of World Records (GBWR) kama mwanamke mwenye miguu mirefu zaidi duniani.

Mwanamitindo huyo wa zamani anayeishi mjini Melbourne, Australia ana miguu yenye urefu wa inchi 51.5 kuanzia kwenye nyonga zake hadi kisigino.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 39 anasema: “Naamini kwamba miguu yangu ndiyo mirefu zaidi nchini Australia kwa kadiri nijuavyo na Amerika pia.”

Kwa mujibu wa GBWR, raia wa Urusi Svetlana Pankratova ndiye kwa sasa anayetambulika kwa kuwa na miguu mirefu zaidi duniani akiwa na miguu yenye urefu wa inchi 51.9 na hivyo kumkaribia.

“Kwa sababu ya ukaribu huo nadhani inafaa kutukutanisha na kuangalia hesabu zinaanzia wapi kupata urefu kamili na kubainisha mshindani asiye na utata,” anasema mama huyo.

Urefu wa Caroline ni futi 6.2, ikimaanisha kwamba miguu yake inachukua asilimia 69 ya umbo lake.

Caroline daima amekuwa akihangaika kusaka nguo zinazoendana na miguu yake mirefu na myembamba na amekuwa akivuta macho ya watu wanaoshangaa kila aendako.

“Lakini mara nyingi nafurahia hali hii. Marafiki zangu daima wanalazimika kujiandaa kidogo wakati tunapotoka pamoja kwa sababu tutavutia macho ya watu, hasa ninapovalia viatu virefu vya mchuchumio,” anasema na kuongeza:

“Kwa sasa iwapo nitatoka na watu jioni, ninatarajia kuvuta macho ya hadhira, ni aina ya maisha ambayo nimeshayazoea.

“Kuna watu wachache tu wanaosema vitu vibaya kuhusu hali hii niliyobarikiwa, lakini sehemu kubwa wanaisifu.”

Lakini Caroline hakuwa daima mwenye kujiamini kwa mwonekano wake huo tangu mwanzo, kwa sababu wakati fulani akiwa msichana mdogo hakuwa akipendezwa na mwonekano wake ambao alijaribu kuuficha.

Anaeleza: “Kuna kipindi sikuupenda urefu wangu, ambapo niliona ni wa kuchukiza na usiovutia. Nilichotaka ni kuwa sawa na wengine.

“Nilianza uanamitindo nilipokuwa na umri wa miaka 15 na hilo likanipa hali ya kujiamini.

“Miguu yangu imeonekana katika matangazo mengi ya stoking (soksi ndefu) lakini pia nilikataliwa katika ajira nyingi kwa sababu ya urefu wangu huu.”

Anasema aliambiwa ni mrefu mno kwa viwango vya urembo vya Australia na hakuweza kuvaa nguo za wanamitindo kwa sababu hazikuwa zikimuenea.

Anabainisha kuwa kadiri alivyopata kazi kutokana na miguu yake, ndivyo pia alivyokataliwa katika kazi nyingine kwa sababu hiyo hiyo.

Caroline anaonekana ameurithisha urefu wake kwa watoto wake kwani mwanae Cooper (13) tayari ana urefu wa futi 6 na inchi 2 na bintiye Zoe (15) ana urefu wa futi 5 na inchi 9.

Mama wa Caroline, Janet Ware, hata hivyo ana urefu wa futi 5 na inchi mbili tu.

“Daima ni mrefu kuliko marafiki zake wote. Ni mama wa aina yake na ninaona fahari kuwa na binti kama huyu,” Janet anasema na kuongeza:

“Huwa nafarijika mno ninapotoka kutembea naye. Mara nyingi hupenda kujivuta nyuma kumwacha atangulie kidogo ili niweze kufaidi mwitikio wa watu kwake.”

Caroline, aliyeolewa kwa mjenzi Cameron, anasema mama mkwe wake hutengeneza nguo na mumewe ameibuni nyumba yao ili iwe na urefu wa futi 10 kwenda juu na jiko la ziada ili kuendana na familia yake ya warefu.

Cameron anasema: “Mimi na Caroline tuna urefu sawa, lakini tunaposimama sambamba, miguu yake ni mirefu kuliko yangu.

“Kwa kumuoa, hakika tumeweza kuendana na urefu na nadhani miguu yake ndiyo mirefu zaidi nchini Australia,” anasema.

“Alikuwa akifanya kazi dukani wakati tulipoonana kwa mara ya kwanza nikawa na mazoea ya kwenda kumuona na yote si kwa sababu ya urefu wake bali kumpenda yeye kama alivyo.”

Watoto wa Caroline wanasema kwamba ndoto yao ni kumuona mama yao anaingia katika Kitabu cha Guinness World Records.

Zoe anasema: “Mama anaonekana mkubwa wa kutisha mithili ya ghorofa refu lililoenda hewani (skyscraper). Tunapokuwa nje kwa mitoko huonekana namna alivyompiku kila mtu kwa urefu.

“Nadhani mama yangu anaonekana mrembo kwa kweli na ninatamani kuwa kama yeye,” anasema.

Iwe atapewa hadhi ya mwenye miguu kuliko wote duniani au la, Caroline anasema anajivunia mwonekano wake.

“Ninaweza kusema kuwa  kama mwanamke mwenye umri wa miaka 39, niko salama kwa jinsi nilivyo, najisikia mrembo kuliko kipindi chote cha maisha yangu,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles