27.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

MWANAMKE ACHAGUA NGO’MBE BADALA YA NDOA

MKAZI wa Jimbo Tamil Nadu nchini India, Selvarani Kanagarasu, amekataa kuolewa ili awe na muda wa kumiliki ng’ombe anayeshiriki michezo ya mapigano ya mafahali.

Kanagarasu (48) alikuwa kijana wakati alipoamua kufuata nyayo za baba na babu yake ambao walifuga ng’ombe wa kiume walioshindana katika michezo ya mafahali maarufu kama Jallikatu.

Jallikatu ni mchezo maarufu kwa karne kadhaa katika jimbo hilo la kusini mwa India na huchezwa wakati wa msimu wa mavuno ufahamikao kama Pongal kila Januari.

Maelfu ya watu hufukuza ng’ombe ili kuchukua zawadi zilizowekwa kwenye pembe zao.

Mchezo huo ulisimama kwa kipindi cha miaka miwili kufuatia marufuku ya Mahakama ya Juu kwa madai kuwa wanyama walifanyiwa ukatili.

Lakini kufuatia maandamano makubwa jimboni humo, Serikali ya jimbo ikaamua kuyaruhusu kuendelea Januari 2017 bila kujali marufuku ya mahakama.

”Baba na babu yangu walifuga ngombe na kuwachukulia kama watoto wao”, alisema.

Jukumu la kuendeleza utamaduni wa kifamilia lilipaswa kuwaangukia nduguze wa kiume, lakini anasema hawakuwa na muda wa kuwaangalia wanyama hao na hivyo akaamua kuchukua jukumu hilo.

Uamuzi wa  Kanagarasu wa kufuga ng’ombe huyo badala ya kuolewa si wa kawaida hususan katika maeneo ya vijijini  India.

Anasema nduguze na watu wa familia yake walishangazwa na hatua hiyo lakini baadaye wakaikubali.

Na ukakamavu wake umemfanya aheshimiwe na familia yake na wanakijiji wengine, huku akiendelea kumfuga ng’ombe huyo anayempatia kipato cha kutosha .

Ng’ombe anayemfuga afahamikaye kama Ramu na ana miaka 18 akiwa amejizolea umaarufu mkubwa katika mchezo huo eneo hilo.

Ramu ameshinda mashindano matano kati ya saba ya Jallikattu, ambayo ameshiriki, akishinda zawadi kama vile sare na sarafu ya dhahabu kwa mmiliki wake.

”Ramu ni mwanangu wa kiume .Alishinda zawadi lakini cha muhimu alinipatia heshima katika kijiji chetu”, alisema akiongezea kuwa Ramu ana upendo mwingi licha ya kimo chake na hasira katika mashindano ya Jalikattu.

Hata hivyo, kwa miaka mingi, watu wengi wamejeruhiwa ama hata kuuawa katika mashindano hayo wakiwamo mashabiki wa mchezo huo.

Alimnunua mnyama huyo wakati alipokuwa umri wa miaka 10.

Mmiliki wake alitaka kulipwa fedha nyingi lakini baadaye akakubali kumuuzia Ramu kwa kiwango cha chini baada ya kumwambia alitaka kumfuga ng’ombe huyo lakini hana kiwango cha fedha anachotaka.

Nyumba yake ndogo ina jiko na chumba kimoja cha kulalia, ambacho pia ndio sebule na eneo, la kulalia.

Yeye hupata kipato cha Rupee 200 ambazo ni sawa na Sh 7,500 kwa siku na anatumia fedha zote kuhakikisha Ramu yu katika hali nzuri.

Mbali na nyasi na matawi ya mchele wanayopewa ng’ombe wengi katika jimbo la Tamil Nadu, pia anakula nazi, tende, ndizi njugu, mtama na mchele.

”Kulikuwa na siku ambapo nilikula mara moja kwa siku ili niweze kuweka fedha za kumnunulia Ramu chakula”, anasema.

Mbali na chakula chake maalum, Ramu huhitaji mazoezi ya kila mara.

Hivyo basi Kanagarasu humchukua kila siku katika kidimbwi cha maji kilichopo kijijini ili aweze kuogelea kwa lengo la kuimarisha magoti yake.

”Binamu yangu Rajkumur pia humtembeza na kumfunza kukabiliana na wapinzani wake katika mchezo wa Jalikattu”.

”Pia hupata ripoti ya hali ya afya ya Ramu kutoka kwa daktari wa wanyama kabla ya kila shindano la Jalikattu ili kuhakikisha kuwa Ramu anafuzu”, anasema

Kutokana na ufanisi wa Ramu katika mashindano ya Jalikattu, watu wengi wamejitokeza kumnunua ng’ombe huyo.

Mmoja wa ndugu zake, Indira Selvaraj anasema alikataa ombi la hadi Rupia 100,000 kumuuza Ramu.

Anataka kumfuga ng’ombe huyo,kumuandaa kwa mashindano ya Jalikattu ndio lengo kuu la maisha yake.

Tulishindwa kumshawishi kukubali ombi letu. Sasa tumekubali kwamba hakuna gharama ya kufuta malengo ya mtu.

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,327FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles