29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanajeshi mstaafu apandishwa kizimbani

o-law-facebook

Na KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MWANAJESHI mstaafu, Salum Kamota (74) na wenzake watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakituhumiwa kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 190 na silaha.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Elia Athanas, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.

Mbali na Kamota ambaye ni mwanajeshi mstaafu mwenye cheo cha meja, washtakiwa wengine ni Rajabu Mwinyimkuu (42), Jumanne Juma (30) na Said Abdallah (36), ambao walisomewa mashitaka sita.

Wakili  alidai   kati ya Januari mosi, 2006 na Septemba, mwaka huu, kati ya mikoa ya Pwani, Tanga na Dar es Salaam, mshtakiwa Kamota alikutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh 162,750,000.

Washtakiwa Mwinyimkuu, Juma na Abdallah wanadaiwa katika kipindi hicho, katika Kijiji cha Ntumbabukang’ondo, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, walikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh milioni 32.5 bila kuwa na leseni.

Juma anadaiwa Septemba 14, mwaka huu, katika eneo la Buguruni, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, alikutwa na kipande kimoja cha meno ya tembo chenye thamani ya Sh milioni 1.3 bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Mshtakiwa Juma anadaiwa kukutwa akimiliki bunduki   ya riffle 375 na 458 bila ya kuwa na leseni ya msajili wa silaha.

Wakili Athanas alidai mshtakiwa Kamota, Septemba 7, mwaka huu, maeneo ya Korogwe, mkoani Tanga, alikutwa na risasi 40 za riffle na risasi nne za bastola bila kuwa na leseni.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote  kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa husikilizwa Mahakama Kuu.

Wakili wa Serikali alidai upelelezi haujakamilika na shauri hilo liliahirishwa hadi Oktoba 13, mwaka huu na washtakiwa walipelekwa rumande hadi tarehe hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles