Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
MWANAHISA wa Kampuni ya Jamii Media, Micke William (27), ameunganishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao huo unaoendesha mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo, katika kesi ya kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi.
William aliunganishwa jana katika kesi mbili zinazomkabili mkurugenzi huyo zilizopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali, Mohammed Salum, akishirikiana na Mwanasheria Mwandamizi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Johannes Kalungula, waliwapandisha washtakiwa hao kizimbani na kuwasomea mashtaka katika kesi namba 456 na 457 za mwaka 2017 zilizopo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa.
Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Simba katika kesi namba 456,2017, Wakili Salum alidai walitenda makosa hayo kati ya Aprili mosi na Desemba 13, mwaka jana, eneo la Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Inadaiwa wakiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media ambayo inaendesha tovuti ya JamiiForums, wakijua Jeshi la Polisi Tanzania linafanya uchunguzi kuhusu mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa katika tovuti yao, kwa kuuzuia uchunguzi huo walishindwa kutekeleza amri ya kutoa data walizonazo.
William na Melo katika kesi namba 457,2017 iliyopo mbele ya Hakimu Mwambapa, wanadaiwa kati ya Mei 10 na Desemba 13, mwaka jana, kwenye eneo la Mikocheni, Melo akiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media, wakijua Jeshi la Polisi Tanzania linafanya uchunguzi kuhusu mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa katika tovuti yao, kwa njia ya kuzuia uchunguzi huo walishindwa kutekeleza amri ya kutoa data walizonazo.