29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAHABARI ALIYEDAIWA KUUAWA AIBUKA

KIEV, UKRAINE


MKOSOAJI wa Serikali ya Urusi, Arkady Babchenko, aliyetangazwa na vyombo vya habari vikikariri taarifa ya polisi na mkewe kuwa ameuawa, ameonekana mjini hapa juzi.

Babchenko alikuwa ametolewa salamu za rambirambi kutoka kila sehemu na jina lake kuongezwa kwenye orodha ya wanahabari waliouawa.

Lakini alirejea kutoka ‘wafu’ akiandamana na mkuu wa ujasusi wa Ukraine na mwendesha mashtaka mkuu.

Mwanahabari huyo alikuwa ametangazwa kuuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake mjini hapa, kitu ambacho kumbe ulikuwa mchezo wa kupangwa.

Babchenko (41) alivishukuru vikosi vya usalama vya Ukraine kwa kuyaokoa maisha yake kabla ya kumwomba radhi mkewe kwa kumuweka katika hali ngumu kama hiyo.

“Nnavyojua ni kuwa operesheni hii ilipangwa kwa zaidi ya miezi miwili, lakini nilifahamishwa mwezi uliopita. Katika mwezi huu niliona jinsi maofisa walivyofanya kazi, kama walivyofukua mambo kama nyati. Tuliwasiliana mara kwa mara, tukatafakari na kukamilisha mipango,” alisema.

Maofisa walifafanua kuwa kitendo hicho cha kuongopa kifo cha mwanahabari huyo kilihitajika ili kuwanyamazisha watu wanaoshukiwa kupanga kumuua mkosoaji huyo wa Serikali ya Urusi.

Lengo lilikuwa ni kukusanya ushahidi zaidi unaomhusisha mtu aliyepewa kazi ya kuendesha mauaji hayo na maofisa wa ujasusi wa Urusi.

Mkuu wa Usalama wa Ukraine, Vasily Gritsak, alidai maofisa wa ujasusi wa Urusi walimpa mwanamume mmoja wa Ukraine dola 40,000 kufanya mauaji ya mwanahabari huyo anayeishi uhamishoni.

Kifo hicho kilipangwa na mwanahabari huyo na polisi wa Ukraine baada ya kupokea vitisho vya kuuawa.

Polisi imesema mshukiwa mmoja amekamatwa.

Rais Petro Poroshenko alisifu habari hizo kama ishara kuwa Ukraine ‘imeupita mtihani wa kuwa nchi huru’ na akaiita siku hiyo kuwa ‘siku ya kuzaliwa’ kwa taifa hilo.

Lakini wakati mamlaka za hapa zikisifu kitendo hicho, nje ya mipaka ya taifa hilo kimeshutumiwa.

Mkuu wa Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka, Christophe Deloire, aliyaita matukio hayo kuwa mabaya mno na ya kusikitisha.

Jukumu sasa lipo mikononi mwa wapelelezi wa Ukraine kuthibitisha kuwa matumizi haya mabaya ya imani ya umma yalistahili.

Watahitaji kuonyesha kuwa kutoweka kwa Babchenko kuliwasaidia wapelelezi kuthibitisha kikamilifu uhusiano kati ya anayetuhumiwa kupanga njama hiyo na maofisa wa ujasusi wa Urusi. Ulimwengu unasubiri hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles