33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAFUNZI UDSM AJIBU MTIHANI  WA KINGEREZA KWA KISWAHILI

Na NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM


MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu (DUCE), amejibu maswali ya mtihani kwa kutumia lugha ya Kiswahili licha ya mtihani husika kuelekeza majibu ya Kiingereza, jambo ambalo limewaweka wakufunzi wake njia panda.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inataja lugha ya Kiswahili na Kiingereza kuwa lugha rasmi za kujifunzia lakini Kiswahili kinatumika kufundishia elimu ya awali na msingi, wakati Kiingereza kinatumika kufundishia katika baadhi ya shule za msingi huku kikiwa ni lazima kwa sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na elimu ya juu.

Ushuhuda huo ulielezwa jana na Mhadhiri wa chuo hicho, Godwin Nko, wakati akichangia mdahalo ulioandaliwa na Shirika la HakiElimu mada ikiwa ni ‘nini mchango wa lugha ya kufundishia na kujifunzia katika kuufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025’.

“Wengine wanazungumzia kuchanganya lugha za kufundishia, utakuta mwanafunzi anaelewa lakini je, tunamfanyia tathmini kwa kutumia lugha gani ama tunampimaje?

“Juzi tumekutana na kihoja, kuna mwanafunzi mmoja ambaye maswali yote amejibu kwa Kiswahili na mtihani ni wa Kiingereza, mpaka sasa hivi tunajadiliana kwamba tutafanya vipi maana sera hairuhusu. Hivyo utaona kwamba kuna shida mahala fulani na hata wanafunzi wetu hata ukiangalia insha zao ni tatizo.

“Tunatakiwa tuwe na ‘intensive program’ ya kufundisha Kiingeraza lakini si ufundishe Historia kwa Kiingereza ukidhani kwamba ndio unaokoa Kiingereza,” alisema Nko.

Ushuhuda mwingine ulitolewa na Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kondo iliyoko Wilaya ya Kinondoni, Daudi Kuboja, ambaye alisema aliwahi kukuta mwanafunzi wa kidato cha pili ameandika mashairi 20 ya mapenzi kwa lugha ya Kiswahili katika daftari la Kiingereza.

“Hiki ni kisa cha kweli kabisa, nilikuwa napita darasani najaribu kuwaambia wanafunzi waongee Kiingereza lakini nikachungulia dirishani nikamwona mtoto wa kike anasoma daftari.

“Nikavizia nikamshtua na kumwambia anipe daftari lake. Nilikuta ameandika mashairi ya Kiswahili. Huyu mtoto si mjinga, kuna vitu anavyo kichwani anaelewa.

“Haina maana kwamba kwenye Kiswahili anapata A lakini kuna vitu anavijua, nilimwambia mwalimu wa kike tusaidiane namna ya kuwalea hawa watoto.

“Labda angekuwa anaongea Fizikia au Historia kwa Kiswahili, anafundishwa kwa Kiswahili huyu anayeweza kumudu kutunga mashairi angeweza hata akaambulia vitu fulani ambavyo vingemfanya ubongo wake ukue na awe mtu wa maana katika jamii,” alisema Mwalimu Kuboja.

Alisema wazazi wengi wamechanganyikiwa wanahofia maisha ya watoto wao baada ya kumaliza shule kwa kudhani kwamba Kiingereza ndio msingi.

Naye Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Martha Qorro, alisema Kiingereza hakitoshelezi kutumika kufundishia na tafiti zaidi ya 20 zimethibitisha hilo.

“Tangu mwaka 1977 mpaka leo tafiti zinaendelea na jibu ni lile lile, inaelekea kama nchi iliyotawaliwa inaendeleza yaleya waliowatawala na ukiuliza unaonekana kama mwanaharakati fulani,” alisema Profesa Qorro.

Mtaalamu wa Lugha, Dk. Michael Kadeghe, alisema bila kutumia lugha za kigeni kasi ya maendeleo itakuwa ndogo kwani hata watoto wengi wanaofundishwa kwa Kiswahili wamekuwa wakishindwa mitihani tofauti na wale wanaofundishwa kwa Kiingereza.

“Maprofesa wanaotetea matumizi ya Kiswahili wanasomesha watoto wao ‘English Medium’ na wengine shahada zao wamesoma katika nchi zinazotumia Kiingereza.

“Kingereza kimefanyiwa utafiti na kimetumika zaidi ya miaka mingi lakini Kiswahili ni kigumu kwa sababu istilahi zinazotumika darasani zinatofautiana na za mtaani…labda istilahi ziongezeke hadi milioni moja ndio Kiswahili kinaweza kutumika kufundishia,” alisema Dk. Kadege.

Kwa upande wake Mwandishi Mkongwe, Jenerali Ulimwengu, alisema hakuna nchi yoyote iliyoendelea duniani kwa kutumia lugha ya kigeni.

“Tusijifanye kama matahira, nchi nyingi zinatumia lugha zao na hatuwezi kuibadilisha nchi hii ikawa ya Waingereza. Ili uendelee ni lazima uwe na jamii inayosoma vitabu na yenye lugha mama,” alisema Ulimwengu.

Mkurugenzi Mwenza wa Taasisi ya Confucius ya UDSM inayofundisha lugha ya Kichina, Profesa Aidan Mutembei, alisema watu wengi wenye shule binafsi ni wafanyabiashara lakini kama wakigundua Kiingereza hakina biashara wataanza kukipigia debe Kiswahili.

“Mapinduzi ya viwanda popote duniani yalikwenda sambamba na mapinduzi ya utamaduni, lazima serikali iwekeze kwenye Kiswahili ili iubebe uchumi na uchumi ukibebe Kiswahili,” alisema Profesa Mutembei.

HAKIELIMU

Mkurugenzi wa HakiElimu, Dk. John Kalage, alisema wanaamini mjadala huo unaweza kuja na majibu ya mkanganyiko unaoendelea kuhusu lugha ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi mbalimbali za elimu hapa nchini.

“Tunaamini mjadala huu ni mwafaka na muhimu ili kutoa nafasi kwa wadau na wananchi kutoa mapendekezo kwa serikali lugha gani inaistahili ya kufundishia na kujifunzia itakayotufikisha katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Dk. Kalage.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Mjadala Wa lugha ya kufundishia haujaanza leobna tafiti nyingi zmefanyika. mimi naona kingereza kitumike kuanzia nursery had chuo kikuu ili wanafunzi wawe na msingi mzuri Wa lugha hyo.pia itawasaidia kuendana na dunia ya sasa ya utandawazi hasa katika ushindani in east Africa and outside Africa.

  2. Si huko tu UDSM suala hilo pia limetokea katika Chuo Kikuu Cha Tumaini Makumira Arusha Baada ya mwalimu mwanafunzi wa mwaka wa tatu kuwasilisha mbele ya wanafunzi wenzake somo ambalo lilipaswa kuwasilisha kwa lugha ya kingeleleza (educational management) na kuliwasilisha kwa lugha ya kiswahili jambo ambalo liliwafanya wanafunzi wengi kutahamaki kwa kitendo kilichofanywa na mwanafunzi huyo na hali hii ilipelekea kunyimwa alama za uwasilishaji na mwalimu wake wa somo la educational management.
    Hivyo kutokana na jambo hili kunaulazima wa kukihalalisha kiswahili kutumika kufundishia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu kwani wanafunzi tuliowengi tumechoka kuwa watumwa wa lugha iliyoletwa na mtubwi iliyowatesa na kuwanyanyasa mababu zetu
    Hivo ombi langu nalielekeza mamlaka husika

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles