29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

‘Mwanafunzi huandaliwa kwa kujengewa msingi mzuri elimu ya awali’

Wanafunzi wa Shule ya Msingi uhominyi iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi uhominyi iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

NA RAYMOND MINJA, IRINGA

CHANGAMOTO kubwa inayoikabili sekta ya elimu nchini ni ubora wa elimu ambao umesababisha kushuka kwa kiwango cha elimu.

Moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni katika elimu ya awali ambayo imeoenekana kutopewa msukumo wa pekee hasa katika maeneo mengi nchini.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa msingi mkubwa wa elimu siku zote huanzia katika ngazi za awali huko ndiko ambako unaweza kuzalisha wanafunzi bora kwani hata wahenga walisema uimara wa nyumba hutokana na jinsi ulivyoandaa msingi.
Mwalimu wa Taaluma katika Shule ya Msingi Uhominyi iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Sifa Mbwete, anasema walimu wa awali ni tatizo katika shule nyingi hali inayosababisha wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao ya kumaliza darasa la saba.

Mbwete anasema watoto wengi wamekuwa wakimaliza shule bila kujua kusoma na kuandika kutokana na maandalizi mabovu waliyopata toka awali yaliyochangiwa na kukosa walimu wenye ujuzi na maarifa ya kutosha.

“Msingi mkubwa wa elimu ni ule unaoanzia chini kabisa, huko ndiko utakakozalisha mwanafunzi mzuri ama mbaya. Mara nyingi watoto hufundishwa na walimu wa msingi ambao hawana mafunzo na matokeo yake ni lazima wataboronga tu,” anasema Mbwete.

Changamoto ya ukosefu wa walimu wa awali ndiyo iliyomsukuma Mkuu wa Chuo cha Ualimu wa Awali kilichoko Nyororo mkoani Iringa (TUSAALE), Taifa Lugson, kukabiliana na uhaba wa walimu wa awali hapa nchini.

Lagson ambaye kitaaluma ni Mwalimu na Mthibiti Ubora wa
Elimu katika Wilaya ya Mufindi, anasema wakati akikagua shule za msingi alibaini kuwapo kwa changamoto kubwa ya ukosefu wa walimu
wa awali jambo lililomsukuma kuanzisha chuo hicho ili
kuzalisha walimu watakaosaidia kupunguza changamoto hiyo.

Anasema hapo awali msingi wa ufundishaji watoto elimu ya awali ulikuwa haupewi kipaumbele hususani vijijini ndio maana baadhi ya wanafunzi walikuwa wakimaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma wala kuandika.

“Kinachotakiwa kwa sasa ni wadau na sekta ya elimu kuwekeza katika elimu ya awali ili nchi iwe na idadi kubwa ya walimu katika ngazi hiyo,” anasema lagson.

Anasema walimu hao ndio msingi mkubwa wa kujenga kizazi chenye uelewa kuanzia ngazi ya chini hadi juu na kutoa wito kwa vijana kusoma masomo ya awali ya ualimu na kuacha kuwategemea walimu wazee.

“Ni ngumu sana kumchukua mwalimu anayefundisha elimu ya msingi kwenda kufundisha elimu ya awali, huwa wanafundisha tu ili mradi, hii si sahihi tunahitaji walimu vijana wasomi walio tayari kufundisha watoto wetu ili tuweze kufuta kabisa suala la mwanafunzi kumaliza darasa la saba akiwa hajui kusoma na kuandika,” anasema.

Stanley Mlomo ni mhitimu wa ualimu wa awali, anasema changamoto kubwa ni upatikanaji wa ajira na kuiomba serikali kuajiri walimu wa awali wenye ujuzi ili kuweza kupandisha kiwango cha elimu hapa nchini.

“Ni jambo la kushangaza kuona serikali ikizalisha wanafunzi ambao hawajui kusoma na kuandika katika karne hii ya sayansi na teknolojia wakati kuna walimu bora wenye ujuzi na ari ya kufundisha watoto wa awali,” anasema Mlomo.

Nasibu Mengele ni Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Iringa, anakiri kuwepo kwa upungufu wa walimu wa awali hatua iliyosababisha kushirikiana na wadau wa elimu kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu wa shule za msingi ili kuweza kufundisha wanafunzi hao.

“Baada ya serikali ya mkoa kuona tatizo ni kubwa iliamua kutafuta njia mbadala ya kutoa mafunzo kwa walimu wa msingi,” anasema.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa waliwapa mafunzo walimu 46, Iringa vijijini 300, Kilolo 234 na Mufindi 353 ili kufundisha darasa la kwanza na la pili.

Hivi karibuni Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bhalalusesa, alisema hadi sasa wamefanikiwa kutoa elimu ya awali kwa asilimia 30 nchi nzima.
Anasema elimu hiyo inatekelezwa nchini kupitia mpango wa Kukuza Stadi za Kusoma (KKK) na lengo lake ni kuboresha elimu kwa wanafunzi.
“Bado tuna changamoto ya ufundishaji wa elimu ya awali kwa sababu shule nyingi za vjijini hazifundishi elimu ya awali tofauti na mjini, hivyo tumeagiza kila shule ya msingi nchini lazima iwe na darasa la elimu ya awali,” anasema Profesa Bhalalusesa.

Anasema katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali imetoa mafunzo kwa walimu 24,156 wanaofundisha elimu ya awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles