Na Ibrahim Yassin-Nkasi
MWANAFUNZI wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Milundikwa wilayani Nkasi, Dickson Selemani (15), mkazi wa Kjiji cha Katani, ameponea chupuchupu kufa baada ya kudaiwa kunywa dawa aina saba tofauti za hospitalini kwa lengo la kutaka kujiua akidaiwa hataki shule.
Akizungumza eneo la tukio jana, mama mzazi wa mtoto huyo, Stella Khamis, alisema tukio hilo lilitokea saa 2 asubuhi, baada ya kumfokea mwanawe kutokana na kutokwenda shule.
“Nilimfokea kwanini hajaenda shule, nilimwamuru aondoke haraka, kumbe yeye akawa amekasirika sikujua, nikaondoka kwenda shambani kuendelea na kazi zangu,” alisema.
Alisema baada ya muda mfupi, mtoto huyo alijifungia ndani na kunywa dawa za hospitalini zilizokuwamo ndani, kisha kuandaa kamba ili kujinyonga.
Akiwa ndani, mmoja wa wana familia aliingia na kumkuta akiwa mahututi kutokana na dawa alizokunywa.
Baada ya hali hiyo, mwanafamilia huyo alitoa taarifa kwa majirani ambao walifika na kumkimbiza zahanati ya kijiji hicho kwa matibabu.
Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Katani, Solana Kazikodi, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema mwanafunzi huyo alijiunga na masomo ya sekondari, baada ya kufanya vizuri mtihani wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Katani, mwaka jana.
Kazikodi alisema tangu kuanza msimu wa masomo mwaka huu, amekuwa na mahudhurio hafifu, jambo ambalo linaonyesha hataki kusoma.
Mganga wa zahanati hiyo, Godfrey Manga alikiri kumpokea mwanafunzi huyo na kumpatia matibabu ambayo yameokoa uhai wake.