28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi aliyefukuzwa shule afaulu mtihani bila kuufanya

Nyemo Malecela -Kagera

ALIYEKUWA mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kalenge, Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, aliyefukuzwa shule kwa madai ya kuwa na ugonjwa ambao anaweza kuwaambukiza wanafunzi wenzake, amefaulu mtihani wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne mwaka jana kwa daraja la pili licha ya kutoufanya.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kagera (Takukuru), John Joseph, jana amesema kuwa tayari wanawashikilia walimu watatu wa shule hiyo ambao ni Mkuu wa Shule, Boniface Eliyaabi, Makamu wake, Edwin Valentine na Edvace Richard kwa makosa ya rushwa, hasa matumizi mabaya ya ofisi kwa kufanya usajili kwa udanganyifu katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka jana.

Joseph alisema walimu hao baada kumfukuza shule mwanafunzi huyo, walimuingiza shuleni mwanafunzi mwingine ambaye alitumia namba ya mtihani ya mwanafunzi aliyefukuzwa kufanyia mtihani huo wa taifa na kufaulu kwa daraja la pili.

“Kibaya zaidi mwanafunzi huyo ambaye aliingizwa kufanya mtihani kwa kutumia namba ya mwanafunzi mwingine ni ndugu wa mmoja kati ya walimu hao.

“Baada ya matokeo kutoka, mwanafunzi aliyefukuzwa aliona amepata daraja la pili wakati huo akiwa hajafanya mtihani. Ndipo hofu ikaanza kwa mwanafunzi huyo ambaye hakufanya mtihani jambo lililomlazimu kushirikiana na baba yake kwenda kutoa taarifa Takukuru Juni 19, 2020,” alisema Joseph.

Alisema kuwa walimu hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika kwa makosa ya kufanya udanganyifu katika mitihani kwa manufaa yao kwa kumfukuza mwanafunzi shule kwa kumsingizia kwamba ni mgonjwa na anaweza kuwaambukiza wanafunzi wengine na kisha wakamwingiza mwanafunzi mwingine ili aweze kufanya mtihani kwa kutumia namba yake ya mtihani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles