25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Mwanafunzi akimbiliakwa ofisa elimu kukwepa ndoa nyumbani

Na LEONARDMANG’OHABUTIAMA

HAPPINESS Stephen (17) ni mkazi wa Kijiji cha Kamgendi, Kata ya Bwiregi wilayani Butiama, Mkoa wa Mara.

Happiness ni mhitimu wa kidato cha nne mwaka huu. Licha ya kuhitimu kidato cha nne, safari yake ya elimu haikuwa nyepesi kutokana na vikwazo mbalimbali ambavyo amekuwa akikumbana navyo kutoka kwa familia.

Kwa kawaida jamii ya Mkoa wa Mara huwa na tabia ya kumtumia mtoto wa kike kama njia ya kujipatia utajiri, mtoto huyu pia ametumbukia katika mkasa wa aina hii, baada ya mama yake mzazi kutaka kumuoza kwa bwana mmoja ikiwa imesalia miezi minne kabla ya mtihani wa taifa uliomalizika hivi majuzi.

Happiness anasema mpango huo wa kuozwa ulitayarishwa na mama yake anayemtaja kwa jina la Elizabeth Stephen, Juni mwaka huu.

Anasema mama yake alipanga kumwozesha kwa kijana mmoja ambaye ni askari, mkazi wa jiji la Dar es Salaam na mzaliwa wa Kijiji cha Kamgendi, anayekadiriwa kuwa na umri usiopungua miaka 33.

Anadai alibaini kuwapo kwa mpango huo baada ya kuona hali inabadilika nyumbani na kisha mama yake mzazi kumweleza kuwa anatakiwa kuolewa, jambo ambalo hakuliafiki kwa sababu alipenda kuendelea na shule ili afikie ndoto yake ya kuwa mwanasheria.

Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya siku iliyopangwa yeye kuolewa, aliamua kutoroka nyumbani na kwenda kutafuta msaada katika ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa wa Mara.

Anadai kwa kuwa hakuwa na fedha za nauli, alitembea kwa miguu kuelekea huko eneo ambalo lina urefu wa zaidi ya kilometa 50.

“Sikuwa namfahamu ofisa elimu wala ofisi yake, ila nilikwenda hadi katika kanisa moja ambalo tulikuwa tunakwenda kuweka kambi kwa ajili ya masuala ya kidini, nilipofika pale nilimkuta askari mmoja, nikamweleza shida yangu akanipeleka kwa ofisa elimu.

“Nilifanya hivi kwa sababu nilitaka kuendelea na shule ili nitimize ndoto yangu ya kuwa mwanasheria.

Ofisa elimu aliniuliza nikamweleza, akampigia Ofisa Elimu Sekondari wa Butiama, Sairis Mtweve, akamwambia hana taarifa,” anasema Happiness.

Baada ya hapo, anasema alilazimika kuishi kwa ofisa elimu huyo wa mkoa kwa muda wa siku nne, kisha kukabidhiwa kwa ofisa elimu wa Butiama ambaye alimpeleka Halmashauri ya Butiama kwa taratibu zingine.

Anasema baadaye alihamishiwa katika Shule ya Sekondari ya Bumangi, ambayo ina huduma ya bweni ili kumwezesha kusoma kwa utulivu.

Anasema hapo aliendelea na masomo yake hadi walipokaribia kufanya mitihani ya kuhitimu, ndipo alipolazimika kurejea katika shule yake aliyoandikishwa (Bumaswa) ili kufanya mitihani.

“Mwanzo hali ilikuwa ngumu kwa sababu sikuwa nimewazoea wanafunzi wala na hata walimu, lakini baada ya mwezi mmoja nilizoea, nikaanza kusoma vizuri. Hapa mazingira ya kusomea yalikuwa mazuri kwa sababu tulikuwa tunaishi pale pale na kulikuwa na vitendea kazi vingine ambavyo Bumaswa hakuna pamoja na maabara,” anasema.

Anasema wakati akiendelea na mitihani yake, ndugu zake walipata taarifa kuwa amerejea shuleni hapo, akafuatwa na kaka yake aliyemtaja kwa jina la Kwangwe Stephen, akamtisha kwa kumuuliza amewezaje kujaribu kumfunga mama yake, huku akimwambia kuwa amejiona mjanja kwa kukataa kuolewa, sasa hana ujanja tena kwa sababu shule inaekelea ukingoni.

Happiness anasema awali wakati mchakato wa kutaka aolewe ukifanyika, kaka yake huyo hakuwapo kwa sababu anaishi Mwanza.

Kutokana na hali hiyo, hadi sasa binti huyo hajaweza kuunganishwa na familia yake kwa kuhofia wanaweza kutumia kipindi hiki cha kusubiri matokeo kumlazimisha aolewe. Hivyo, amepewa hifadhi na mmoja wa watumishi wa halmashauri hiyo.

Ofisa elimu wilaya

Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Butiama, Sairis Mtweve, anathibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Anasema baada ya kupata taarifa hiyo alimuita mama mzazi wa binti huyo ili kufahamu kiini cha tukio, lakini mama huyo alikataa na kusema mwanawe alirubuniwa kanisani alikokuwa akisali.

Anasema baada ya mama huyo kukataa alimweka rumande kwa siku moja kisha akamwita tena kwa mahojiano, ambapo wakati huu alieleza ukweli na hivyo kumtaka achangie gharama za mtoto huyo kuhamishwa shule ikiwamo kusaidia kupata sare za shule na chakula, gharama ambazo hata hivyo hakuweza kuzitoa badala yake alichangia Sh 100,000 tu.

“Mimi mwenyewe nililazimika kumshonea sare za shule, nikampeleka Bumangi Sekondari na changamoto kubwa ilikuwa ni chakula, kama mnavyofahamu shule ile haihudumiwi na Serikali ni wazazi ndio wanaopaswa kutoa chakula,” anasema Sairis.

Mkuu wa wilaya hiyo, Anna-Rose Nyamubi, anaahidi kumsaidia binti huyo kuhakikisha anafikia ndoto zake na kwamba hata asipofaulu kuendelea kidato cha tano ataangalia namna ya kumwendeleza.

“Mimi ni mwalimu nimefanya kazi kwa miaka 15, ninalea watoto wa watu hadi sasa. Nitamsaidia huyo binti hata kama hataendelea zaidi kielemu, atakuwa kati ya watu nitakaowapigania waende JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) ili akirudi apambane na wanaomlazimisha kuolewa,” anasema Mkuu huyo wa wilaya.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bumangi, Kyangwe Leonard, anasema kwa kipindi ambacho binti huyo amekaa shuleni hapo alibadilika kitaaluma japo kwa kiasi kidogo ikilinganishwa na wakati anaanza masomo.

“Hali yake kitaaluma ilibadilika kidogo kwa sababu ya mazingira aliyoyakuta yalimsasaidia kusoma kwa bidii, alipata muda wa kusoma na kudhibitiwa kinidhamu. Naweza kusema alibadilika kidogo kwa sababu ya muda na msingi aliokuja nao, muda aliokaa ni mfupi kielimu lakini na msingi aliokuja nao ulikuwa ni mbovu,” anasema Leonard.

Anasema awali hakuwa na nidhamu ya kuridhisha, pengine kutokana na mazingira aliyotoka ya shule ya kutwa, japo walijitahidi kumbana ili aendane na mazingira hayo mapya.

Mkuu wa Shule yaSekondari Bumaswa, Safari Sabuni, hakuwa tayari kuzungumzia suala hili kwamadai kuwa alihitaji ruhusa aidha ya ofisa elimu au Mkuu wa Wilaya, Anna-RoseNyamubi.

Mama mzazi

Mama mzazi wa binti huyo, Elizabeth Stephen, anasema huo ni mchezo uliotengenezwa na kijana mmoja kijijini kwao, baada ya binti yake kuwa anatumia muda mwingi kukaa kanisani badala ya kwenda shule hivyo, baada ya kuhoji kwanini binti huyo anatumia muda mwingi kanisani bila kwenda shule wakaamua kueneza uvumi kwamba alitaka kumuoza.

Anasema kijana huyo ndiye aliyemwelekeza binti yake kwenda kwa ofisa elimu kwa madai kuwa anatakiwa kuolewa.

“Mtoto alikuwa anashinda kanisani, haendi shule nikimuuliza anasema anafanya maombi, sasa ndugu zake wengine wakubwa wakaniuliza mbona huyo mtoto kila siku anashinda hapo wakati ni mwanafunzi? Nikakasirika nikamzuia kwenda kanisani kwa wiki mbili, waliposikia hivyo wakatengeneza njama wakamweleza kuwa nataka aolewe.

“Niliitwa, ikanibidi ninyenyekee, wakaniweka ndani wakanipa na masharti, wakanitaka nitoe fedha ili mtoto aende shule nikatoa, na hata akiwa shuleni alikuwa ananipigia simu namtumia fedha ya matumizi,” anasema Elizabeth.

Kaka wa binti huyo

Kangwe Stephen ambaye ni kaka wa Happiness, anasema Elizabeth ni mke mdogo wa baba yake hivyo amekuwa akimshirikisha katika mambo mengi ya kifamilia kwa sababu ni miongoni mwa maelekezo aliyoachiwa na marehemu baba yake wakati wa uhai wake.

Anasema wakati binti huyo anarejea Bumaswa kujiandaa na mitihani, yeye alikuwa nyumbani mapumzikoni hivyo, alielezwa na mdogo wake mwingine aliyekuwa anasoma shule moja na binti huyo kwamba amerejea shuleni na kuna gharama za usafiri alitakiwa kuzilipa.

Stephen anasema baadae Mkuu wa shule hiyo, Safari Sabuni, aliwataka kulipia gharama za usafiri alioutumia binti yao na akazilipa.

“Ni jambo la kumwomba Mungu, hawa watoto kuna wakati wanaweza kukugeuka kabisa. Kama amefikia hatua hiyo sasa naamini kile ambacho mama alidai kuwa amepewa tuhuma zisizo za kweli,” anasema Stephen.

Anasema kinachofanywa na binti huyo ni upotoshaji mkubwa kwa sababu mama yake anapambana kwa kila hali kuhakikisha watoto wake wanasoma.

“Huwezi kuamini huyu mama anapiga hadi kokoto ili watoto wasome, hivi mtu wa hivyo anaweza kutaka mtoto wake aache shule aolewe? Hawa watoto ni changamoto, wakisharubuniwa wako tayari kumsaliti hata mzazi.

Anaongeza kuwa mgogoro huo ulianza baada ya ndugu zake wengine kupinga tabia za mdogo wao kushinda kwa kijana mmoja waliyekuwa wakisali wote, akimsaidia kazi huku akiacha kwenda shule hivyo, wakamshawishi kwenda kwa ofisa elimu kudai kwamba familia ilimtaka aolewe.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,875FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles