23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

MWAMUNYANGE: SITOSAHAU MILIPUKO YA MABOMU

Mwandishi Wetu –Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, amesema katika kipindi chake cha utumishi jeshini, hatasahau kamwe tukio la milipuko ya mabomu kwenye vikosi vya Mbagala mwaka 2009 na Gongolamboto mwaka 2011.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya kuapishwa mkuu mpya wa majeshi, Jenerali Venance Mabeyo, Jenerali mstaafu  Mwamunyange alisema tangu aingie jeshini mwaka 1971, wakati wa milipuko hiyo iliyosababisha vifo na uharibufu wa mali, ndiyo ulikuwa mgumu zaidi kwake.

“Wakati wa milipuko ya Mbagala na Gongolamboto nilikuwa kwenye nafasi hii (Mkuu wa Majeshi), huu ndiyo ulikuwa wakati mgumu kwangu kwa sababu ilisababisha vifo, mali za watu na askari ziliteketea, kwangu kipindi kile kilikuwa kigumu sana,” alisema Mwamunyange.

Milipuko ya mabomu ya Mbagala, iliyotokea Aprili 2009, mbali na kusababisha majeruhi lukuki, takribani watu 20 walikadiriwa kupoteza maisha.

Kwa upande wa Gongolamboto, ilitokea Februari 2011 na pia ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 19, huku mamia wakijeruhiwa.

Kwa upande wake, Jenerali Mabeyo alisema kazi ya jeshi hilo ni kulinda mipaka ya nchi na watu wake, jambo aliloahidi kulisimamia.

Alisema Jenerali mstaafu Mwamunyange alifanya mambo mengi, hivyo yeye na wenzake wataanzia alipoishia.

MAZUNGUMZO YA JPM NA MWAMUNYANGE

Kwa upande wake, Rais Dk. John Magufuli baada ya kumwapisha Jenerali Mabeyo, alisema wakati anaondoka nchini kwenda Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU), Jenerali mstaafu Mwamunyange alimweleza kuwa muda wake unakwisha, lakini hakutaka kuteua mtu mwingine kwa wakati huo.

“Nilivyokuwa naenda AU kwenye mkutano, nadhani ilikuwa tarehe 14, Mwamunyange aliniambia ‘unajua muda wangu unaisha tarehe 31, naomba uteue mtu mwingine’, nikasema nikiteua leo watasema nimekutumbua kwa sababu muda wako bado haujaisha, pia mimi nasafiri ninayekufahamu ni wewe, sasa nikiteua mtu mwingine na hizi siku nne zitakazokuwa zimebaki… (kicheko ukumbi mzima), nikasema mzee endelea tu mpaka nitakaporudi nchini,” alisema.

Alisema wakati akiwa Ethiopia, viongozi wa nchi nyingine wakawa wanamuuliza nani atakuwa mkuu wa majeshi ajaye, hali iliyomfanya kufahamu kwamba nafasi hiyo ni nyeti.

Mbali na suala hilo, Rais Magufuli alitaka majeshi yote yawe mfano kwa kuhakikisha nchi inakuwa ya viwanda kwa kuanza kuhakikisha sara zote za majeshi haziagizwi kutoka nje.

“Siyo kila kitu kununua kutoka nje, lazima tujipange hii dhamira ya Tanzania ya viwanda itokee jeshini,” alisema.

Akizungumzia ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es hadi Morogoro, alisema Serikali ya Tanzania itagharamia kwa asilimia 100 na baada ya mwezi mmoja mkandarasi atakuwa eneo la kazi.

Alisema baadhi ya watu wanadhani fedha za ujenzi huo zinatoka Uturuki jambo ambalo halina ukweli kwa sababu taifa hilo linatoa wakandarasi tu.

Magufuli alisema kukamilika kwa reli hiyo kutaruhusu treni za umeme ama mafuta kupita na zitakuwa na uwezo wa kutembea kilomita 160 hadi 180 kwa saa.

Alisema Aprili, mwaka huu, zabuni ya kujenga kipande kingine cha reli hiyo kutoka Morogoro hadi Dodoma itatangazwa.

Mbali na kuapishwa kwa mkuu mpya wa majeshi, pia Rais Magufuli alimwapisha Luteni Jenerali James Mwakibolwa kuwa Mnadhimu Mkuu.

WAKUU WA MAJESHI WALIOPITA

Mabeyo anakuwa mkuu wa majeshi wa nane tangu mwaka 1964.

Wengine ni majenerali Mrisho Sarakikya (1964-1974), Abdallah Twalipo (1974-1980), David Musuguri (1980-1988), Ernest Kiaro (1988-1994), Robert Mboma (1994-2002), George Waitara (2002- 2007) na Mwamunyange aliyehitimisha utumishi wake mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles