Theresia Gasper -Dar es salaam
KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi, amemrejesha Hassan Mwasapili katika kikosi hicho, huku akimsajili Aaron Kalambo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Awali, Mwasapili alikuwa akikipiga Mbeya City kabla ya kusajiliwa na Azam FC msimu wa mwaka 2018/19 ambako mkataba wake umemalizika na kurejea tena katika timu yake hiyo ya zamani.
Baada ya kuondoka Mbeya City na kutua Yanga, Mwambusi alinaswa na Azam akiwa msaidizi wa Hans van der Pluijm ambao walifungashiwa virago kutokana na timu hiyo kupata matokeo yasiyoridhisha msimu uliopita.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwambusi alisema anaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao kwani anahitaji kutengeneza kikosi chenye ushindani.
“Tumeanza mazoezi, hii ni wiki ya pili sasa na tumefanya usajili kwa wachezaji chipukizi ambao naamini wataisaidia timu pamoja na wazoefu kama watatu ambao ni Kalambo na Mwasapili,” alisema.
Alisema katika siku hizi kadhaa zilizosalia, watacheza mechi za kirafiki kama tano ili kuendelea kuwaangalia wachezaji wake na kuwaweka fiti zaidi.
Mwambusi alisema mechi hizo zitampa mwanga wa kuanza vizuri ligi wakiwa wamejiandaa kwa ushindani.