JINA la kocha msaidizi wa timu ya Yanga, Juma Mwambusi, limeonekana kuchukua nafasi katika timu ya African Lyon, baada ya kocha wake mkuu, Bernardo Tavares, kuonekana akifanya mambo yanayoshabihiana na ya kocha huyo.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya kumalizika kwa mchezo wa African Lyon dhidi ya Toto Africans, uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutofungana.
Baada ya mchezo huo, kocha wa African Lyons, Tavares, aliwazuia wachezaji wake kuondoka uwanjani huku akiwataka wengine waliokuwa jukwaani kuvaa jezi na kuanza kufanya mazoezi kwa pamoja.
Kitendo hicho ndicho kilichoibua hisia za uwepo wa Mwambusi katika timu hiyo, kutokana na programu hiyo mara nyingi kutumiwa na kocha huyo kipindi akiinoa Mbeya City na kuipa mafanikio katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mashabiki wa soka waliojitokeza uwanjani hapo walisikika wakisema kuwa utaratibu huo unamsaidia mchezaji kuwa fiti zaidi, lakini makocha wengi wanaofundisha Tanzania wamekuwa hawautumii.
“Mchezaji anapomaliza kucheza na kufanya mazoezi mepesi kabla ya kwenda kupumzika humfanya kuwa fiti zaidi, kwani hata kama kuna mahali pameshtuka panakaa sawa, tofauti na akipelekwa kupumzika moja kwa moja.
“Utaratibu huu ni Mwambusi pekee ndiye aliyekuwa akiutumia akiwa na Mbeya City na ndiyo maana wachezaji wake kila mara walionekana moto wa kuotea mbali,” alisema Salehe Majuto, ambaye alikuwa uwanjani kushuhudia pambano hilo.