Mohamed Kassara -Dar es salaam
KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi ametamba kuhakikisha anairudisha timu hiyo kwenye chati, kama ilivyokuwa msimu wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo walimalimza wakiwa nafasi ya tatu.
Mwambusi amerejea tena katika kikosi hicho, akirithi mikoba iliyoachwa na Mrundi, Ramadhani Nsanzurwimo aliyeifundisha klabu hiyo kwa misimu miwili.
Mwambusi aliipandisha Mbeya City daraja ikitoka Ligi Daraja la Kwanza na kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza , msimu wa 2013/14.
Klabu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Mbeya ilikuwa tishio kwa vigogo wa soka nchini, Simba,. Yanga na Azam.
Kutokana na mafanikio yake katika Ligi kuu msimu wa kwanza tu, nyota wengi wa klabu hiyo waliweza kuzivutia klabu mbali mbali, ambapo zilijitosa kuwasajili.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwambusi alisema timu hiyo itarudi kivingine msimu ujao, kwa ajili ya kuhakikisha inarudisha heshima yao iliyopotea kwa miaka sita katika ligi hiyo.
Alisema katika kuhakikisha hilo, wameamua kurejea kwenye sera ya usajili ya kukusanya vijana wenye vipaji kutoka Mbeya, kama walivyofanya wakati timu hiyo inapanda Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2013.
“Tupo katika mikakati mizito ya kuhakikisha timu yetu inarejea katika ubora wake, uongozi pamoja na wakazi wa Mbeya kwa ujumla tunapaswa kuunganisha nguvu ili tufikie malengo hayo.
“Tumefanya usajili wa kulingana na mapungufu yetu, katika suala la usajili tumerudisha sera yetu ya kutumia vijana wa nyumbani ambao walitupa mafanikio makubwa wakati tunakuja Ligi Kuu, tunajua Mbeya kuna vipaji vingi sana, na kwa muda mrefu havijatumika ipasavyo,”alisema kocha huyo msaidizi wa zamani wa Yanga na Azam FC.