32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mwalimu Nyerere: Miaka 19 baada ya kifo chake (3)

Na Mark MwandosyaHII ni sehemu ya tatu ya hotuba ya Profesa Mark Mwandosya kwa Chuo Kikuu cha Comoro wakati wa Maadhimisho ya Miaka 19 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Moroni, Comoro, Oktoba 26, 2018.

Katika sehemu ya pili wiki iliyopita pamoja na mambo mengine mwanzidshi aliendelea kuangazia harakati za kupigania uhuru zikiwa tayari mikononi mwa chama cha TANU pamoja na imani za mwana TANU. Sasa endelea…

Imani hizi zinajumuisha vipengele ambavyo vinapaswa kulenga kuumba au kuchochea maadili ya Taifa.

Nilikuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Majengo, shule ya watoto wa Kiafrika katika moja ya vitongoji vilivyotengwa kwa Waafrika cha Majengo wakati Jumamosi moja jioni nilipoandamana na baba yangu kwenda kuhudhuria mkutano wa umma uliofanyika katika kituo cha ustawi cha kitongoji kingine cha weusi lakini kilichokuwa pekee Mjini Mbeya.

Ulikuwa mkutano wa kwanza wa kisiasa niliohudhuria. Hata katika hatua za awali za maisha tulisikia kuhusu Nyerere, kuhusu kauli mbiu: Uhuru Sasa na mwito kwa Waafrika kuiunga mkono TANU katika harakati za kupigania uhuru.

Mtu aliyevutia umati hakuwa mwingine zaidi ya Julius Nyerere. Kitu cha kwanza nilichovutiwa na Nyerere aliyevalia kawaida shati jeupe la mikono mirefu na suruali ya khaki akishikilia fimbo  ya kutembelea katika mkono mmoja, kilikuwa mfanano usio wa kawaida na baba yangu.

Kwa kuhudhuria kwetu mkutano huo, baba yangu alivunja sheria ya utumishi wa kikoloni.

Kama mwajiliwa wa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki baba yangu alipigwa marufuku kuwa mwanachama wa taasisi ya kisiasa na hakuruhusiwa kushiriki shughuli yoyote inayoweza kuelezwa kuwa ya kisiasa”.

Lakini bado nyumba yetu haikuwa na zaidi ya siasa. Kwa baba yangu na wafanyakazi wenzake baada ya saa za kazi walishiriki mijadaa isiyokwisha ya siasa wakati wakinywa “kimpumu”, pombe ya kienyeji iliyotengenezwa kutokana na mtama.

Chumba chetu cha kupumzika kilijaa vitabu, magazeti na majarida ya ndani na nje ya nchi.

Tabia yangu na moyo wa kusoma vitabu na magazeti na kufuatilia masuala ya karibuni na dunia nilirithi kutoka kwa baba yangu.

Wazo la hotuba yake Nyerere, alilolitoa kwa Kiswahili rahisi lilikuwa kwamba sisi Waafrika tumetawaliwa kwa muda mrefu na kuwa hatupaswi kuwa raia wa daraja la tatu katika nchi zetu wenyewe na bara letu, na kwamba wakati umefika kwa wakoloni kufungasha virago na kuondoka.

 

Watendaji wa TANU na Nyerere walifahamu kwamba kila neno alilozungumza litarekodiwa na kupitishwa katika Tawi Maalumu, idara ya polisi inayohusika na usalama na inteljensia.

Hakukuwa na maofisa wa kikoloni katika mkutano huo, ikimaanisha kwamba tawi maalumu lilikuwa na Waafrika miongoni mwao na hufanya kila linaowezekana kupenya kuingia ndani ya TANU. Kwa kuhofia usalama kama watendaji wa chama walivyokuwa, Nyerere kamwe hakukaa hotelini au nyumba za wageni.

Badala yake alikaa katika maeneo ya siri ya wanachama waaminifu wa TANU.

Tunafahamu kwamba katika kitongoji cha Mjini Mbeya, alikuwa mgeni wa mara kwa mara wa Binti Matola, kada mtiifu wa TANU kutoka familia ya Yao, ambayo ilihamia Tanganyika kutoka kusini mwa Nyasaland (sasa Malawi).

Bado sijafahamu iwapo Binti Matola, ambaye soko kuu Mjini Mbeya limepewa jina lake, alihusiana na Cecil Matola, rais mwasisi wa African Association (AA).

Kila alipokuja Mbeya wakati wa miaka ya harakati za kupigania uhuru, Nyerere alikaa na familia ya Binti Matola, Familia ya Mama Mwashambwa au Familia ya Mzee Kissoki.

Alikuwa daima akiambatana na mpigania uhuru John Mgogo Mwakangale.

Imani ya Mwana TANU lilikuwa wazo la Nyerere. Kwa namna alivyo mnyenyekevu, kamwe hakukubali sifa hiyo. Kwa viongozi wengine kama yeye miongoni mwa waasisi 20 wa TANU ni pamoja na watu wa kariba ya Joseph Kasella Bantu,  Abdulwahid Sykes, John Rupia na wengineo.

Ili nisitoke nje ya mada ya kongamano hili wakati nikihutubia mkutano huu katika kituo cha juu zaidi cha elimu, Chuo Kikuu cha Comoro, napenda kuendelea kujikita katika imani namba moja ya TANU, Yaani binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja; na ile namba tatu; Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma; Rushwa ni adui wa haki na ile namba saba; Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote; Nitatumia umoja wa Afrika kuangazia mchango wa Nyerere kwa ukombozi wa Afrika hasa Mashariki na Kusini mwa Afrika. Pia nina nia ya kujadili mchango wa Nyerere kwa ukombozi wa kimawazo kwa kuondokana na ujinga na kufuata elimu na matumizi ya ujuzi uliopatikana.

Nyerere na Ukombozi wa Elimu

Daima ilikuwa imani ya Nyerere kuwa elimu si tu silaha muhimu kabisa ya kuondoa ujinga, pia sharti muhimu katika vita dhidi ya maradhi na uondoaji umasikini.

Wakati mtu anaposoma maandishi ya Nyerere, anatambua bila shaka yoyote juu ya uhusiano kati ya elimu, ujuzi, ukombozi wa mawazo na malengo yote yakubalikayo ya elimu katika jitihada za binadamu kuondokana na vikwazo vya asili na vile alivyowekewa na binadamu wenzake (kama vile, kudhibiti na kusimamia mazingira). Ushuhuda wa Mwalimu kuhusu ukuu wa elimu kwa maendeleo utakuwa umechochewa na makuzi yake, miaka ya awali, elimu ya  sekondari, elimu ya juu, harakati za kupigania uhuru na aina ya jamii aliyotokea

Itaendelea wiki ijayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles