Na ELYA MBONEA
-ARUSHA
Mwalimu mstaafu Fatuma Pyuza (57), aliyekuwa akifundisha Shule ya Msingi Mlimani, Monduli mkoani Arusha, amemuomba Rais Dk. John Magufuli aingilie kati madai yake ya malipo ya kufungia mizigo baada ya kustaafu.
Akizungumza na Mtanzania Digital mjini hapa, Mwalimu Pyuza, amesema alipaswa kulipwa fedha hizo tangu Februari 17, mwaka 2017.
“Ninazungushwa kila siku nalazimika kusafiri kutoka Singida kwenda Monduli hii ni safari ya sita, kila nikipiga simu kwa Ofisa Elimu anadai eti anashughulikia.
“Walimu wengine wamelipwa iweje mimi nizungushwe, namuomba Rais Dk. Magufuli aingilie kati, nimetumia gharama kubwa kufuatilia hadi sasa,” amesema mwalimu huyo.
Mtanzania Digital lilipomtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli, Steven Ulaya, kuzungumzia madai ya mwalimu huyo amesema hawezi kukataa kama hadai ama la ingawa hajawahi kumuona.
“Mshauri aje anione ofisini, ndiyo ninaloweza kukwambia kwa sasa,” alisema DED Ulaya.