27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalimu arejesha fedha za wanafunzi

Na Abdallah Amiri, Igunga

MWALIMU wa Shule ya Sekondari Igunga Day, mkoani Tabora, aliyedaiwa kuwachangisha wanafunzi wa kidato cha tatu zaidi ya Sh milioni 2.8 kwa ajili ya kwenda mbuga za wanyama Ngorongoro kujifunza, ameanza kurejesha fedha hizo.

Hatua hiyo imefikia hapo siku chache baada ya gazeti hili kuripoti juu ya mwalimu huyo, Paulo Msabila kukusanya kiasi hicho cha fedha.

Akizungumza na gazeti hili juzi Mkuu wa Shule hiyo, Nelson Edward alisema Mwalimu Msabila alionekana Desemba mwishoni mwaka jana, ambapo alikubali kuzilipa fedha zote alizokuwa amewachangisha wanafunzi mwaka jana na kuzitumia tofauti na kazi iliyokusudiwa.

Mkuu huyo wa shule alibainisha kuwa, hadi sasa zaidi ya Sh milioni moja tayari amewalipa wazazi wa wanafunzi waliotoa fedha hizo. Ambapo kila mwanafunzi alikuwa akitoa Sh 50,000 na ameahidi kumalizia kulipa fedha zote Februari mwaka huu.

Hata hivyo Edward alidai pamoja na kulipa fedha hizo tayari yeye kama mkuu wa shule ameishamwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Rustika Turuka kwa ajili ya kumchukulia hatua za kiutumishi.

Amewataka walimu wengine kutojiingiza katika vitendo kama hivyo alivyofanya Mwalimu Msabila.

Nao baadhi ya wazazi ambao bado hawajalipwa fedha zao Rashidi Mgendi na Petronila Joseph wameiomba Serikali kumchukulia hatua kali mwalimu huyo ili iwe fundisho kwa baadhi ya walimu wengine wenye tabia kama hiyo.

Sambamba na hayo gazeti hili lilifanya juhudi za kumtafuta Mwalimu Paulo Msabila kupitia simu yake ya kiganjani ili kujua kiwango ambacho ameshalipa lakini kwa muda wote simu yake ilikuwa haipatikani.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Igunga, Dk. Dalali Peter Kafumu amemtaka mwalimu huyo kurudisha mara moja fedha hizo kwa wazazi kwa kuwa kitendo hicho ni cha wizi, ambacho hakiwezi kuvumiliwa.

“Mimi kama Mbunge siko tayari kufumbia macho kitendo kama hiki kwa kuwa na mimi nilichangia Sh 100,000 kwa maslahi ya wanafunzi, lakini huyo mwalimu aliamua kuzitafuna hizo fedha, hivyo nitachukua hatua za kibunge dhidi ya mwalimu huyo endapo mkuu wa shule na mkurugenzi watashindwa kulishughulikia suala hili,” alisema Kafumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles