27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwakyembe awataka viongozi TFF wajiuzulu

Bethsheba Wambura, Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amewataka viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kujiuzulu.

Amesema iwapo uamuzi wao wa kumsimamisha kazi aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike waliiga kutokana na kile walichokifanya chama cha Soka nchini Misri inabidi viongozi wote wa shirikisho hilo kuachia ngazi.

Nchini Misri, Rais wa Chama cha Soka cha nchi hiyo (EFA), Hani Abou Rida alijiuzulu na benchi zima la ufundi baada ya kumfuta kazi aliyekuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa, Janvier Aguirre kutokana na kutolewa kwa timu hiyo katika michuano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), nchini humo, ambapo walitolewa na Afrika Kusini katika mechi iliyochezwa Julai 7 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Julai 11, Waziri Mwakyembe amehoji utaratibu upi ulitumika wakati wa kumfukuza Amunike na kama waliiga kutoka Misri basi waige kila kilichotokea nchini humo.

“Sijui msingi wa kumuondoa Amunike ni upi, si kwamba mimi nilikuwa namtaka wala simhitaji, lakini nataka kila kitu kiende kwa utaratibu na ndiyo maana nataka kuwahoji msingi wa kumuondoa Amunike ni upi?

“Hatupingi kilichotokea ila mpango wa TFF ni upi kutupeleka hatua nyingine, au tunaiga kilichotokea Misri, kama tunaiga basi tuige sawa sawa, kwamba baada ya kumwambia kocha aondoke inabidi na wewe kiongozi wa shirikisho na wenzako muondoke muwape watu wengine,” amesema Mwakyembe.

Aidha, Waziri Mwakyembe alionesha kukerwa baada ya kuwaita baadhi ya viongozi wa TFF katika kikao na hawakutokea badala yake wakatuma wawakilishi.

“Nimeambiwa kwamba ana vikao vingine, ndiyo unaweza kuona kiburi cha viongozi wa soka hapa nchini, unaitwa na Serikali una vikao vingine badala yake unatuma wasaidizi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles