Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amewaonya watu wanaopiga picha kwa simu mara tu zinapotokea ajali na kusambaza mitandaoni.
Mwakyembe ametoa onyo hilo leo Jumanne Julai 9, wakati wa shughuli ya kuaga miili ya wafanyakazi wa Azam Media waliofariki jana Julai 8, katika ajali ya gari kati ya Shelui na Igunga na kuongeza kuwa Sheria ya Makosa ya Mitandao chini ya kifungu Na. (23), inazuia kufanya hivyo.
“Watanzania nawaomba sana tuendeleze tabia yetu ya utu bila hata ya kutumia sheria, ndugu zetu wanapopata ajali pamoja na kwamba kila mtu sasa hivi ana uwezo wa kununua simu nawaombeni sana acheni tabia ya kupiga picha na kurusha mitandaoni, hufikirii kuwa hao unaowapiga picha wana ndugu, marafiki na watoto.
“Sheria inazuia na tutakufunga na nafikiri hili ni onyo la mwisho na hatutaongea tena,” amesema Dk. Mwakyembe.