25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MWAKYEMBE AIBU

Na AGATHA CHARLES

RAIS Dk. John Magufuli amesema ameshangazwa na kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ya kupiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote bila kuwa na cheti cha kuzaliwa.

Takribani saa 72 zilizopita daktari huyo wa sheria, Mwakyembe wakati akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro, alisema Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuwa na takwimu sahihi za wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kupanga mipango ya kimaendeleo sambamba na kuzuia wageni kuingia nchini kinyemela.

Akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi kabla ya kuondoka Ikulu ya Chamwino, Dodoma na kurejea jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe kwamba Serikali imepiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote, iwe za kidini, kimila na kiserikali bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kinachotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kuanzia Mei mosi, mwaka huu, ilimshtua hivyo alilazimika kutoa ufafanuzi na kuifuta.

“Mimi nilivyosikia jana (juzi) eeh! nilishangaa, nilishangaa na kweli nilishangaa na ndio maana na nyinyi mmeniwahi asubuhi hapa najiandaa kwenda Dar es Salaam na nyinyi mmeshangaa,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Katika ufafanuzi huo, Rais Magufuli ambaye si mara ya kwanza kutofautiana au kutengua maagizo ya wasaidizi wake, alisema ingawa yeye si mwanasheria lakini anafahamu sheria ya vizazi na vifo sura ya 108 iliweka masharti ya usajili wa lazima kati ya mwaka 2009, lakini hakukuwa na kipengele cha kuoa au kuolewa.

“Na mimi nimesikia kama ninyi mlivyosikia, sielewi vizuri, mimi sio mwanasheria lakini ninachojua mimi ile sheria ya vifo na kuzaliwa nafikiri sura namba 108 ambayo iliweka masharti kwenye mwaka 2009 kama sikumbuki, masharti ya kwamba awe na compulsory registration (usajili wa lazima) katika masharti hayo hapakuwapo na kipengele cha kuoa au kuolewa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema katika sheria ya ndoa sura namba 29, hakuna mahali panapozungumza kwamba wakati wa kuoa lazima uwe umesajiliwa.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, pamoja na kutambua umuhimu wa kusajili, takwimu zinaonesha Watanzania wenye vyeti vya kuzaliwa hadi sasa hawafikii asilimia 20.

Alisema suala la kupata vyeti vya kuzaliwa ni muhimu lakini kuwanyima haki ya kufunga ndoa Watanzania takribani asilimia 80 hadi wawe na vyeti vya kuzaliwa ni tatizo.

“Mimi nafikiri hili limetolewa wakati si mwafaka na kwa sababu si mwafaka, mimi kama kiongozi wa nchi ambao walinichagua (wananchi) waendelee katika utaratibu wao wa kawaida lakini kama kuna kifungu cha sheria ambacho kinalazimisha hivi, nitamwelekeza Mwakyembe aende bungeni akakifanyie amendment (marekebisho) kwa sababu yeye ndiye Waziri wa Sheria,” alisema Rais Magufuli.

Rais alisema maisha ya kawaida ya Watanzania hasa vijijini yanajulikana hivyo kulazimishwa kuwa ifikapo Mei mwaka huu wakitaka kuolewa au kuoa kuwa na cheti ni sheria ya kuwabagua Watanzania.

Aliwataka Watanzania kutokuwa na wasiwasi kwani sheria za kubaguana hazitapewa nafasi katika utawala wake.

Rais pia aliwataka wanasheria wa Serikali kuziangalia sheria hizo mbili yaani ile ya vizazi na vifo ya namba 108 na sheria ya ndoa ya namba 29 ili zisilete mkanganyiko kwa wananchi.

“Nafikiri ni vyema pia wanasheria wetu wakaziangalia hizi sheria zetu mbili, sheria ya birth and death registration act cap 108 na sheria ya ndoa cap namba 29 ili waangalie vinavyoenda pamoja ili tusilete mkanganyiko kwa wananchi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema miaka ya nyuma hakukuwa na nyeti vya kuzaliwa kwani vilianza kutolewa baada ya nchi kupata Uhuru hivyo wengi wenye umri mkubwa hawana na kwamba si ajabu hata Dk. Mwakyembe hakuwa nacho.

Katika hoja hiyo, Rais Magufuli alimhoji Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana (50), ikiwa anacho cheti cha kuzaliwa ambaye alisema hakuwa nacho.

“Sasa RC huyu hana cheti cha kuzaliwa je, akitaka kuoa? Maana yake azuiliwe? Kuna ndugu zetu Waislamu anaweza akaoa mwaka huu, akaoa tena baada ya muda, wanatakiwa kuwa na wake wanne, unamzuia asioe? Mfano huyo ni RC hana. Najua ni compulsory (lazima) kupitia kifungu 108, ni sawa watu waanze kutafuta hivyo…nina uhakika hakuna kifungu, kwa sababu na mimi nilikuwamo humo mwaka 2009 nilikuwa waziri,” alisema Rais Magufuli.

Alisema katika sura ya 108, hakuna kifungu kinachozungumzia kuunganishwa na suala la ndoa.

“Hakuna kifungu hapo 108 kinachozungumza kwamba kimekuwa paged na ndoa, ni compulsory (lazima) kuwa registered (kusajiliwa) lakini hiyo compulsory ya 108 hakuna mahali ambako pako paged na ndoa, kwamba usipokuwa na cheti hicho huwezi kuoa au kuolewa hapo sasa umeingia cap 29,” alisema Rais Magufuli.

Alisema suala hilo ni la kisheria zaidi lakini katika utawala wake hawezi kuruhusu kutumika.

“Kama kuna sheria ya namna hii ambayo tuliweza kuiweka kuwa mtu usiposajiliwa maana yake hakuna kufunga ndoa, itakuwa sheria ya ajabu na mimi kama rais wenu siwezi kulikubali kwa wakati wangu. Registration (kusajiliwa) ni muhimu lakini ukishaanza kuingilia mambo ya ndoa haya unawazuia watu kuoana, watu wamezaliana kijijini porini unawazuia mpaka registration, hiyo nayo itakuwa sheria ya kibaguzi sana,” alisema Rais Magufuli.

 

MAMBO AMBAYO MAGUFULI AMEPATA KUWAPINGA WASAIDIZI WAKE

 

Februari 12, mwaka huu, Ikulu Dar es Salaam baada ya kuwaapisha baadhi ya watendaji akiwemo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, Rais Magufuli alitoa takwimu tofauti na zilizotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuhusu idadi ya Watanzania waliokamatwa nje ya nchi na kufungwa katika magereza mbalimbali kwa kosa la dawa za kulevya.

Alisema Watanzania 1,007 walikamatwa ikiwa ni tofauti na idadi iliyotolewa na Waziri Mkuu wakati akihitimisha bunge la mwezi Februari ambapo alitaja idadi inayofikia zaidi ya 578.

Siku hiyo pia Rais Magufuli pasipo kutaja jina, lakini kauli yake ilijenga hisia kwamba huenda alimlenga Waziri wake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema hakuna mtu anayehusika na dawa za kulevya ambaye ataachwa zaidi akisema anashangaa wengine wanasema kuna watu wamejenga majina yao kwa muda mrefu.

Kabla Rais hajatoa kauli hiyo, aliyesikika akitaka busara itumike kutokana na baadhi ya wasanii waliotajwa katika sakata la dawa za kulevya kutumia gharama kubwa kujijengea umaarufu wao ni Nape.

Agosti 26, 2016 Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga katika maeneo ya Kariakoo kwa sababu wanaleta usumbufu na uchafu.

Hata hivyo, Desemba mwaka huo huo, Rais Magufuli aliagiza wafanyabiashara hao wasibughudhiwe na wasiondolewe katika maeneo ya katikati ya miji wanayofanyia biashara kwani hakuna sheria inayowazuia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles