24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mwakinyo afunguka ushindi wake

Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo, amesema hajaridhishwa na ushindi alioupata dhidi ya Mfilipino, Arnel Tinampay kutokana na ubora wa mpinzani wake na changamoto aliyokutana nayo.

Katika pambano hilo lisilokuwa la ubingwa la raudi 10, uzito wa Kilogram 69, lilipigwa juzi  Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Matokeo ya pambano hilo, yalimshuhudia Mwakinyo akishinda kwa pointi.

Licha ya Tinampay kuanza kwa kasi lakini Mwakinyo alifanikiwa  kushinda baada ya jaji wa kwanza kutoa  pointi 97 -93 , wa pili pointi 98-92, huku jaji wa tatu akitoa pointi  96-96. 

Akizungumza baada ya pambano hilo, alisema kilichompa nguvu ni Watanzania waliojaa  uwanjani kushudia mchezo huo, lakini mpinzani wake alikuwa mvumilivu na asiyekubali kushindwa kirahisi.

Mwakinyo pia alisema alikutana na changamoto nyingine ya ‘gloves’,kutokaa vizuri mikononi, hatua iliyosababisha ashindwe kumdunda mpinzani wake mapema.

“Sijaridhika na ushindi niliopata, glove nilizotumia sijazizoea, zimenisumbua,hata  ya mkono wa kulia ilikuwa haijakaa vizuri, ilikuwa inanipa ugumu, sijacheza kwa uhuru kabisa.

“Pia mpinzani wangu ni bondia mvumilivu sana, na ndicho kilichombeba lakini nadhani hajakutana na  watu wanaujua ngumi sawa sawa,” alisema Mwakinyo.

Hata hivyo alieleza kuwa,  amejifunza kupitia pambano hilo kwani anafahamu mabondia wengi wa Tanzania wanapigwa kirahisi watapopanda ulingoni nchi ya nchi.

“Tofauti na uvumilivu, mpinzani wangu alikuwa anajua kabisa nikirusha ngumi nataka kulenga wapi, kitu kinachomfanya hajihami haraka, nadhani hiki kitu nimekichukua kama funzo kwangu kwamba ujasiri unahitajika,” alisema.

Mwakinyo alisema lengo la pambano hilo  ni kuwaonyesha  wadau wa michezo changamoto zilizopo katika masumbwi, hivyo alitoa ombi kwa wadau kujitokeza kuwekeza.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, amepongeza Mwakinyo kwa ushindi  huo.

Mwakyembe alisema hajawahi kuona mashabiki wengi wakijaza uwanja kiasi hicho kutazama mchezo wa ndondi.

“Mwakinyo amevunja rekodi ya kujaza watu, pia nimeona vipaji vingi vya ngumi, kama wizara tutatafuta jinsi ya kuviendeleza, kitendo hiki cha watu kujaa ni ishara tosha kuwa mchezo huu unapendwa.

“Hii ni fursa kwa wafanyabiashara, kampuni kudhamini mchezo huu, sisi tuliopo ndani ya wizara tunajua tunawekeza kiasi gani kuweza kuendelea mchezo huu,” alisema Mwakyembe.

Alisema walitumia miezi sita kutengeneza mfumo mzuri wa kuendesha ngumi za kulipwa kwa kuanzisha kamisheni inayosimamia mchezo huo.

“Mafanikio yameanza kuonekana kwani mabondia zaidi ya sita wamefanikiwa kuleta mikata kutoka nje ya nchi,”alisema Mwakyembe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles