Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), imemfungia bondia Hassan Mwakinyo kutojihusisha na mchezo huo ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja na kumpiga faini sh. 1milioni kwa kitendo cha kugoma kupanda ulingoni Septemba 29,2023.
Katika pambano hilo la IBA Intercontinental, Mwakinyo alitakiwa kupanda ulingoni , jijini Dar es Salaam kupigana na bondia Julius Indongo kutoka Nambia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 10,2023, Katiba Mkuu wa (TPBRC), George Silas uamuzi wa kumfungia bondia huyo umetokana na kikao cha Kamati ya Nidhamu ya misheni hiyo kilichofanyika Oktoba 5, mwaka huu.
Silas amesema kamati ilisikiliza maelezo ya pande zote mbili na vielelezo vyao lakini wakabaini alicholalamikia Mwakinyo hakikuwa kwenye makubaliano ya mkataba wake na promota aliyeandaa pambano hilo, Godson Karigo.
“Mwakinyo amepewa adhabu hii kutokana na kukiuka taratibu za mkataba. Hata hivyo anaruhusiwa kukata rufaa ndani ya siku saba kuanzia leo,”amesema Silas.
Aidha amefafanua kuwa adhabu hiyo pia imetolewa kama fundisho kwa kuwa Mwakinyo ni bondia mkubwa anayetakiwa awe mfano wa kuigwa na kuheshimu viongozi wake.