Na Hadia Khamis, Wetu, Mtanzania Digital
Mwakilishi wa Wastaafu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Stephen Lazaro ameitaka jamii kuendelea kuiamini mamlaka hiyo kwani inauwezo mkubwa wa kutoa wanafunzi waliobobea katika fani mbalimbali.
Akizungumza wakati alipotembelea katika banda hilo liliopo katika maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Lazaro amesema Veta imeendelea kuboresha na kubuni vitu mbali mbali siku hadi siku.
“Jamii iendelee kuiamini Veta kwa kushirikiana nao lakini pia kwa kuleta wanafunzi ili kuweza kupata mafunzo yenye ubora yatakayoweza kuwasaidia kuweza kujiajiri wenyewe.
“Sisi ni wastaafu wa miaka mitano iliyopita lengo hasa la kutembelea Veta ni kwa sababu tumeitumikia lakini tumefurahi kuona jitihada za ubunifu zilizofanywa na wanafunzi pamoja na walimu wao,” amesema Lazaro.
Ameongeza kuwa kwasasa Veta inatumia teknolojia inayotumika viwandani ili kutoa wanafunzi waliobobea kwenye mafunzo ya viwanda.