Na Gurian Adolf-Kalambo
KAYA 47 zimebaki bila makazi baada ya nyumba 13 kubomoka kutokana na mvua iliyonyesha juzi katika Kijiji cha Kasitu, Kata ya Sopa, Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya tukio hilo, wakazi wa kijiji hicho walisema mvua hiyo ilikuwa kubwa na iliyoambatana na upepo mkali.
Anold Yolam, mkazi wa kijiji hicho, alisema baadhi ya watu ambao nyumba zao zimebomoka, wamepewa hifadhi kwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji na wengine kwa majirani na kuiomba Serikali iwasaidie.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Gasper Kateka, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zimebomoka wamepewa hifadhi kwa mwenyekiti wa kijiji na wengine kwa majirani wakati wakisubiri msaada zaidi.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, John Sizo alisema wananchi wengine ambao hawakupatwa na janga hilo wana wajibu wa kuwasaidia watu waliopatwa na maafa hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Just Binyura, alisema tukio hilo limetokana na wananchi kutojenga nyumba imara na zenye ubora.
Alisema nyumba nyingi zilizoathirika hazikuwa zimejengwa kwa kufuata taratibu za ujenzi, hivyo wananchi wanapaswa kuwashirikisha wataalamu wa halmashauri ili wawape ushauri wa namna ya kujenga nyumba bora.