30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mvua yakata mawasiliano Dodoma, TMA yaonya

Pg 1RAMADHAN HASSAN, Dodoma na LEONARD MANG’OHA Dar es Salaam

MAGARI zaidi ya 1,500 jana yalikwama kwa zaidi ya saa 10 eneo la Chalinze Nyama Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na kusababisha adha kubwa kwa abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kanda ya Ziwa na wale wa kutoka Dodoma kwenda Morogoro na Dar es Salaam.

Pia inasemekana baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Nzali Kata ya Hombolo, Wilaya ya Chamwino hawana mahali pa kuishi, kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji.

Msongamano mkubwa wa magari katika eneo hilo ulikuwa zaidi ya kilomita 10 kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua iliyonyesha kuanzia juzi jioni na kusababisha barabara kujaa maji  na njia  kushindwa kuonekana.

Pia mvua hiyo ilisababisha miundombinu ya umeme hususani nguzo zinazosambaza umeme katika kijiji hicho kwenda wilayani Kongwa kuanguka na kusababisha umeme kukatika usiku huo.

Mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) walionekana wakifanya juhudi za kurekebisha hali hiyo ili zisianguke katika maeneo ya watu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alifika katika eneo hilo kujionea hali halisi na kuwataka madereva kuchukua hadhari pindi wanapopita kwenye maeneo yaliyojaa maji.

Rugimbana pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhama kwani mvua bado zipo na zinaendelea kunyesha.

Mkazi wa eneo hilo, Asha Athumani alisema mvua hiyo  ilianza saa 3:00 usiku hadi asubuhi ambayo imeharibu pia miundombinu ya barabara pamoja na ya umeme.

Mkazi mwingine Musa Matonya alisema maji  yalikuwa yakitiririka  kwa nguvu kutoka maeneo ya milimani Kata ya Hombolo na kujaa barabarani.

”Maji yalianza kujaa barabarani na maeneo ya kuzunguka nyumba zetu ikatubidi kukaa nje maeneo ya mwinuko hasa kina mama na watoto wao wadogo pamoja na wazee”alisema.

Barabara hiyo  ilifungwa kwa muda kuanzia saa 12:00 alfajiri hadi saa 8 alasiri baada ya maji kupungua ndipo yaliporuhusiwa kuendelea na safari.

“Ilipofika saa nne nne hivi kuna basi lilijaribu kupita lakini likaserereka abiria wakatokea madirishani baada ya hapo hakuna gari ambalo limeruhusiwa kupita mpaka sasa”alisema Liberatus Manyasi mkazi wa kijiji hicho.

Familia ya mama na watoto wanne iliyodaiwa ni ya Sheikh wa Msikiti wa Jumuiya ya Kiislamu ya Ahmaddiyya uliopo jirani na barabara itokayo Dodoma kwenda Dar Es Salaam nyumba yao  ilizungukwa na maji na kuifanya familia hiyo kushindwa kutoka nje hadi askari wa kikosi cha zima moto kutoka Dodoma Mjini walipokwenda  kuwanusuru.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema serikali itahakikisha wananchi walioathirika wanapata msaada na huduma zote muhimu.

Katika hali ya kushangaza wafanyabiashara wa eneo hilo wametumia hali hiyo ya mafuriko kupandisha bei ya bidhaa mbalimbali yakiwamo maji ambayo awali yalikuwa yakiuzwa Sh 500 hivi sasa yanauzwa Sh 1000 huku sahani moja ya chakula ikiuzwa kati ya Sh 3000 na 4000.

TMA yatahadharisha

Wakati huo huo, Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) imewashauri wananchi kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka hiyo katika kipindi hiki cha mvua za masika.

Ushauri huo umetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa TMA Dk. Hamza Kabelwa wakati wa mazungumzo na MTANZANIA ofisini kwake.

Akizungumzia kuhusu mvua zilizoanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, Dk Kabelwa alisema kuna uwezekano mkubwa wa kuwapo kwa mvua nyingi.

Alisema mvua hizo ni zile zilizozidi wastani katika baadhi ya mikoa ikiwamo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Nyanda za Juu Kusini pamoja na Kanda ya Ziwa Viktoria.

Alisema hadi sasa hali ya mvua katika maeneo mengi ya nchi ni nzuri isipokuwa Nyanda za Juu kumekuwapo na mtawanyiko wa mvua usio mzuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles