20.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Mvua yakata mawasiliano Arusha, Kilimanjaro kwa saa sita

ELIYA MBONEA-ARUSHA

Mvua iliyonyesha kwa takribani saa 10, imezua taharuki katika Jiji la Arusha huku mawasiliano kati yake na Moshi yakikatika kwa saa kadhaa.

Jana katika Jiji la Arusha makazi mengi yalikuwa yamezungukwa na maji huku barabara zikiwa zimejaa maji hali iliyokwamisha wanafunzi na watu wengine kwenda kwenye shughuli zao.

Pia wakati wasafiri waliokuwa wakitoka Arusha kuelekea Moshi na Dar es Salaam walikwama tangu alfajiri jana hadi majira ya saa nne maji yalipopungua barabarani na magari kuanza kupita.

Kukwama kwa wasafiri hao kulisababishwa na Mto Biriri kufurika maji.

Kwa upande wa mafuruko kwenye Jiji la Arusha, mbali na kufurika katika maeneo ya watu, kwenye baadhi ya maeneo watu waliripotiwa kusombwa na maji.

Mmoja wa waliosombwa ni kijana mmoja aliyechukuliwa na maji kwenye mtaro eneo la Kijenge ambaye alisaidiwa na askari waliokuwa wakiongoza magari katika eneo hilo.

Katika mazingira yasiyotegemewa, kijana huyo aliyekuwa akijaribu kuvuka mtaro mkubwa, alijikuta akiteleza na kuanza kusombwa na maji kwa umbali wa hatua 20 kabla ya kuokolewa.

Hata hivyo, mara baada ya kusaidiwa kutoka kwenye maji, kijana huyo aligoma kujitambulisha majina yake na akasujudu akimshukuru Mungu kwa kumwokoa na kifo.

Kutokana na mvua hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi hasa wanapokuta maji mengi barabarani.

Alisema katika maeneo waliyotembelea kujionea hali halisi, hakuna madhara ya kifo yaliyojitokeza zaidi ya uharibifu wa vifaa vya ndani kama makochi, vyombo, magari kuangukiwa na kuta za nyumba na miti kuanguka.

“Saa 7 usiku, Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo alinipigia simu kunipa maelekezo ya kuingia barabarani kuhakikisha tunashirikiana na Zimamoto kuokoa watu na mali zao.

“Nashukuru wananchi wametupa ushirikiano mkubwa, na askari wa Zimamoto kwa uhakika wamefanya kazi kubwa ya kuvuta maji yaliyojaa maeneo yaliyozingira makazi ya watu,” alisema RPC Shana.

Kwa upande wake, Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Arusha, Kennedy Komba, alisema chanzo kikubwa cha maji hayo kusimama na kuingia kwenye makazi ya watu ni njia za maji nyingi kufungwa.

“Niwaombe watendaji wa mitaa na kata tusimamie na kutimiza wajibu wetu, wakati watu wanapojenga tuhakikishe njia za maji hazifungwi ili kupunguza maafa wakati wa mvua kubwa.

“Niwaombe wananchi katika kipindi hiki kukitokea maafa yoyote yanayohitaji uokozi, naomba tuwasiliane kwa namba 114 kwani tukipata taarifa hizi kwa wakati zinaweza kusaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao,” alisema.

 Naye Mkazi wa Mtaa wa Osunyai Ngusero, Emmy Proper ambaye nyumba yake ilizingirwa na maji na kusababisha uharibifu mkubwa wa masofa, vyombo vya umeme  na magodoro, alisema maji yalianza kujaa ndani usiku.

“Tumeingiliwa na maji usiku, hatukulala hapa imebidi tuhamishe watoto mtaa mwingine kuanzia saa 9 usiku, hali ilikuwa mbaya sana, maji yalijaa mpaka usawa wa madirisha,” alisema Emmy.

Mkazi mwingine wa eneo la Kijenge Kati, Kirenga Swai aliyeharibikiwa magari yake mawili na nyumba kujaa maji, alisema saa 12:30 asubuhi alistukia kuona gogo kubwa likisukumwa na hadi kwenye ukuta kisha ukavunjwa na maji kujaa ndani.

“Magari yangu mawili yameharibika kama unavyoona vioo vimepasuka, taa za magari zimevunjika, maji yamejaa ndani, kila kilichomo humo kimejaa matope hakifai tena, vifaa vya umeme vimeharibika,” alisema Swai.

Aidha wakati hali ikiwa hivyo, katika baadhi ya mitaa ya Jiji la Arusha na maeneo jirani hali ilikuwa mbaya zaidi kutokana na magari kushindwa kupita barabarani kutokana na maji kujaa.

Barabara ya Moshi-Arusha hali haikuwa nyepesi kutokana na maji yakiwa na matope mazito kujaa eneo la King’ori na maeneo mengine na kusababisha magari mengi kupita kwa tahadhari.

Licha ya magari kushindwa kupita barabarani kutokana na maji mengi, kwa baadhi ya wakazi wa Jiji la Arusha hali haikuwa rahisi kwani wengi wao walishindwa kufika makazini kwa wakati kutokana na maeneo yao kujaa maji.

Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za mjini Arusha nao walijikuta wakipata wakati mgumu wa kufika mashuleni kutokana na magari yao kukumbwa na kadhia hiyo.

Baadhi yao walishindwa kutoka majumbani mwao kutokana na nyumba kujaa maji, madaftari kulowana na hivyo kushindwa kwenda shuleni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,595FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles