29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Mvua ya dakika 45 yaleta maafa

Na IBRAHIM YASSIN-MBOZI

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha kwa dakika 40 wilayani hapa, imesababisha nyumba 56 kuezuliwa huku watu tisa wakijeruhiwa.

Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Utambalila, Kata ya Nambizo wilayani Mbozi mkoani Songwe.

Mbali na maafa hayo, pia mali kadhaa ziliharibiwa.

Akizungumza jana na gazeti hili, mmoja wa waathirika hao, Simwinga Mwashambwa alisema alfajiri ya jana walisikia mirindimo na vishindo vikubwa na walipotoka nje walikuta mabati yanapeperushwa na upepo, kuta zikianguka, mazao yaliyotunzwa vyote vikizama majini.

Alisema baadaye walitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na kushauriana wakimbilie katika shule ya msingi iliyopo kijijini hapo.

“Kwa sasa tunahitaji msaada zaidi ili tuweze kujenga nyumba na kurudi kwenye makazi yetu maana hata mazao tuliyotunza kwa chakula na mbegu yameharibiwa na maji ya mvua, tunahitaji msaada wa haraka,’ ’alisema Mwashambwa huku akitokwa na machozi.

Ofisa Mtendaji Kata ya Nambizo, Elson Mkwama alisema majeruhi tisa wamepelekwa hospitali na hali zao  zinaendelea vizuri.

Alisema Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo na kamati yake ya ulinzi na usalama wanaendelea kufanya tathmini ya awali kujua ukubwa wa tatizo na jinsi ya kutatua.

Naye Mkuu wa Moa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nickodemas Mwangela alikiri kuwapo maafa hayo.

Mwangela alisema nyumba 56 zimeezuliwa na watu tisa  kujeruhiwa baada ya mvua iliyoambatana na upepo mkali kunyesha ndani ya dakika 40 huku mazao mengi yakiharibiwa na watu hao kukosa makazi.

Alisema kwakuwa huu ni msimu wa kilimo wamewapatia waathirika hao mahema kwa ajili ya kuweka kambi pamoja na mbegu za muda mfupi za mazao ya chakula ili wapande haraka waweze kujipatia chakula.

“Ni tukio baya lililotokea, lakini tunatakiwa kuwahamasisha wakazi wa eneo hili na maeneo mengine wapande miti kupunguza kasi ya upepo maana bila kuchukua tahadhari tutaendelea kukumbwa na maafa kila mwaka,” alisema Mwangela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles